Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa Ndugu Maganya Fadhiri Rajabu akiwa katika mradi wa maji baada ya kuwasili leo tarehe 30 machi 2026 Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma kujionea hatua zinazoendelea katika mradi huo 
Na Regina Ndumbaro Songea -Ruvuma
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Ndugu Maganya Fadhiri Rajabu, leo Machi 30, 2026 amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi mkubwa wa maji wa miji 28 unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) katika Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.
Ziara hiyo imelenga kujionea hatua za utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati unaolenga kumaliza changamoto ya maji safi na salama kwa wakazi wa mji huo.
Akiwasilisha taarifa ya mradi, Mkurugenzi Mtendaji wa SOUWASA, Mhandisi Patrick Kibasa, amesema mradi huo ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kuboresha huduma za majisafi na usafi wa mazingira katika miji 28 nchini.
Ameeleza kuwa mkataba wa utekelezaji ulisainiwa Machi 10, 2022 kati ya Wizara ya Maji na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), huku ujenzi ukianza rasmi Januari 2, 2024 na kufikia asilimia 6.5 ya utekelezaji hadi sasa.
Kwa mujibu wa Kibasa, mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 145.77 unahusisha ujenzi wa miundombinu muhimu ikiwemo kidaka maji katika mto Njuga, mtambo wa kisasa wa kuchuja na kutibu maji wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 16 kwa siku, pamoja na matanki matatu ya kuhifadhi maji yenye ujazo wa lita milioni 9 kwa jumla.
Aidha, zaidi ya kilomita 60 za mabomba ya kusafirisha na kusambaza maji zinajengwa, sambamba na ukarabati wa mtambo wa Matogoro ili kuongeza ufanisi wa huduma.
Ameongeza kuwa hatua zilizofikiwa ni pamoja na usanifu wa miundombinu, ujenzi wa matanki mawili katika maeneo ya Maji Wilaya na Chandamali, pamoja na ujenzi wa tanki la Mahilo lenye ujazo wa lita milioni 5 ambao umefikia asilimia 70.
Hata hivyo, amebainisha changamoto ya mabadiliko ya chanzo cha maji kutoka bwawa lililopangwa awali hadi mto Njuga kutokana na sababu za kiufundi, jambo lililoathiri ratiba ya utekelezaji wa mradi.
Akizungumza katika ziara hiyo, Maganya amesisitiza umuhimu wa wananchi kuwa na subira na kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa mafanikio.
Amesema juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan zinaendelea kuimarisha huduma za maji nchini, akibainisha kuwa lengo ni kufikia upatikanaji wa maji kwa asilimia 100 mijini.
Kwa upande wao, wananchi wa Mahilo akiwemo Abubakary Kawelea, Casian Luoga na Maria Ndunguru wameishukuru Serikali kwa mradi huo na kuomba mkandarasi aharakishe utekelezaji ili kuondoa kabisa changamoto ya maji katika Manispaa ya Songea.







Social Plugin