Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI NANAUKA AZINDUA DAWATI LA HUDUMA KWA VIJANA, AAGIZA BAJETI MAALUM KOTE NCHINI


Na Lulu Mbwaga, Mwanza

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amesema wizara hiyo inaongozwa na falsafa ya kufanya kazi kwa kasi, viongozi kufikika kwa urahisi na matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma.

Kutokana na mwelekeo huo, wizara imeanzisha Dawati la Huduma kwa Vijana litakalopokea maoni, changamoto na mapendekezo ya vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza Februari 19, 2026 katika ufunguzi wa Jukwaa la Vijana (Vijana Platform) mkoa wa Mwanza, Nanauka alisema mfumo huo utawasaidia vijana kuunganishwa moja kwa moja na Maafisa Maendeleo ya Vijana katika mikoa na halmashauri ili kupata msaada wa kitaalamu pamoja na taarifa za fursa zilizopo.

Aidha, amezielekeza sekretarieti za mikoa na halmashauri zote nchini kutenga bajeti maalum kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya vijana katika maeneo yao. Alisema hatua hiyo itaimarisha utekelezaji wa majukwaa ya vijana na kuongeza ushirikiano kati ya serikali na wadau wa maendeleo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, aliishukuru serikali kwa kuendelea kuwainua vijana wa mkoa huo.

Alisema vikundi viwili katika wilaya za Ilemela na Nyamagana vimepatiwa mkopo wa shilingi milioni 200, hatua aliyoitaja kuwa ni chachu ya maendeleo ya vijana.

Makilagi aliongeza kuwa endapo serikali itaendelea kuwekeza kwa vijana katika sekta ya ufugaji, hususan ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, uchumi wa Mwanza utaimarika zaidi kwa kuwa kwa kiasi kikubwa unategemea sekta ya uvuvi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitwima Youth Group, Suzana Lazaro, aliishukuru wizara kwa kuwapatia mkopo wa shilingi milioni 100 kwa ajili ya mradi wa ufugaji wa samaki kwa vizimba, akiahidi kuwa kikundi chao kitakuwa mfano wa kuigwa kwa mafanikio ya kiuchumi na kupambana na umaskini.

Naye kijana Ranford Waya, aliyeshiriki kongamano hilo, aliwahamasisha vijana wenye mawazo ya kibiashara kujitokeza na kushirikiana na wizara hiyo, akisisitiza kuwa serikali ipo tayari kuwainua vijana wenye bidii na maono.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 ni takribani milioni 20.6, sawa na zaidi ya theluthi moja ya Watanzania wote. Takwimu hizi zinaonesha wazi kuwa mustakabali wa Taifa unategemea nguvu, maarifa na ubunifu wa vijana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com