Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATUHUMIWA SABA WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA DAWA ZA KULEVYA SAME

Watuhumiwa saba wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Same, Februari 19, 2026, wakikabiliwa na mashtaka mbalimbali yanayohusiana na dawa za kulevya aina ya mirungi, huku mmoja wao akiwekewa amri ya kuwa chini ya uangalizi wa Polisi kwa miaka mitatu.

Kwa mujibu wa taarifa za mahakama, kesi saba zimefunguliwa, kila moja ikiwa na mtuhumiwa mmoja. Watuhumiwa wote walisomewa mashtaka yao na kukana tuhuma zinazowakabili.

Katika mashauri yaliyosikilizwa mbele ya Mheshimiwa Christanta Chitanda, Hakimu Mfawidhi, watuhumiwa Athuman Tuarira Kivuma, Goodluck Bariki Mungulu na Nuru Mbonea Mndeme wamepangiwa kurejea mahakamani Februari 24, 2026.

Goodluck Mungulu anakabiliwa na shtaka la kupatikana na mirungi yenye uzito wa kilo 1.8. Shauri lake lina dhamana, lakini ameshindwa kutimiza masharti yaliyowekwa.

Athuman Kivuma anashtakiwa kwa kusafirisha mirungi kilo 27, huku Nuru Mndeme akituhumiwa kusafirisha mirungi kilo 25.

Katika mashauri yaliyosikilizwa mbele ya Mheshimiwa Hellen Hozza, Hakimu Mkazi Mwandamizi, watuhumiwa Youze Eliwaha Kitua, Ahadi Mbazi Mnjama na Edson Elihazina Kibaja walikana mashtaka yao.

Youze Kitua, anayekabiliwa na shtaka la kusafirisha mirungi kilo 34, atarejea mahakamani Machi 2, 2026.

Ahadi Mnjama, anayeshtakiwa kwa kusafirisha mirungi kilo 26, amepangiwa Machi 3, 2026.

Edson Kibaja, anayekabiliwa na shtaka la kusafirisha mirungi kilo 24, naye amepangiwa Machi 3, 2026.

Kwa upande wa kesi ya saba, Mganga Wahidi Dorovu alipandishwa mahakamani kwa ajili ya kuwekewa amri ya kuwa na tabia njema (binding over). Mahakama iliamuru awe chini ya uangalizi wa Polisi Same kwa kipindi cha miaka mitatu na kuripoti kituoni kila mwezi, kwa masharti ya kutojihusisha na uhalifu wowote, ikiwemo biashara au matumizi ya dawa za kulevya.

Hatua hiyo inaendelea kuonyesha juhudi za vyombo vya dola katika kukabiliana na biashara na usafirishaji wa dawa za kulevya katika Wilaya ya Same na maeneo jirani.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com