Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAHABARI WASHAURIWA KUJISHUGHULISHA NA KILIMO ,UFUGAJI





Na Mwandishi Wetu, Lumuma Mpwapwa

Ule usemi wa “kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi” umejidhihirisha kwa mwanahabari mkongwe Barnabas Kisengi (Babu), ambaye amejikita katika shughuli za kilimo na ufugaji huku akishughulika pia na uandishi wa habari jijini Dodoma. 

Njia yake ya kipekee imemsaidia kupata kipato cha ziada na kukidhi mahitaji madogo ya kila siku.

Akizungumza na Malunde Blog leo February 28,2026 Dodoma Kisengi ameeleza kuwa licha ya kazi yake ya habari, amekuwa akitumia muda wake wa ziada kulima shamba lake lililoko Lumuma, Jimbo la Kibakwe, Wilaya ya Mpwapwa, ambapo anajishughulisha na kilimo cha vitunguu maji, vitunguu swaumu, maharagwe, muhogo, malimau, ndizi na maembe.

 Anaona mafanikio hayo kama msingi wa kuwekeza katika shamba kubwa siku za usoni.

“Nimekuwa nikitumia muda wangu wa ziada nje ya tasnia ya habari kuingia shambani. Japo nimeanza na shamba dogo, mafanikio yake yananitia moyo na naamini siku moja nitawekeza eneo kubwa zaidi na kuwa mkulima mkubwa,” amesema Kisengi.

Mbali na kilimo, Kisengi anajihusisha pia na ufugaji wa kuku wa mayai na ng’ombe wa maziwa katika makazi yake ya Chinyoyo, Kata ya Ekurilimani. 

Kupitia ufugaji huu, anapata mayai na maziwa kwa familia yake na kuuza kwa wananchi, jambo linaloongeza kipato chake na kusaidia kuendesha maisha ya nyumbani.

 Anaongeza kuwa mtu akishughulika na kilimo au ufugaji huwezi kuamini kuwa ni mwandishi wa habari mjini – hii ni njia ya kujipatia uhakika wa kifedha.

Kisengi ametoa wito kwa waandishi wenzake kuhakikisha wanakuwa na vyanzo vingine vya mapato nje ya uandishi wa habari, kama kilimo, ufugaji au biashara ndogo ndogo, ili kuongeza ustawi wao kiuchumi. 

Amefafanua kuwa kutumia muda wa ziada kwa shughuli hizi ni njia ya kujenga uhakika wa kifedha, kupunguza utegemezi na kuongeza heshima katika jamii.

Kwa ujumla, mwandishi huyu mkongwe anashauri wenzake wasiishie kutegemea tasnia ya habari pekee, bali watumie muda wa ziada kuendeleza shughuli mbadala zinazowainua kiuchumi na kuwawezesha kufanikisha maisha bora kwa familia na jamii yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com