Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAANDISHI WA HABARI WAHIMIZWA KUANDIKA HABARI ZA UCHUNGUZI KUCHOCHEA UWAJIBIKAJI NA MABORESHO YA SERA



Na Bora Mustafa,Arusha.

Waandishi wa habari za mazingira Kanda ya Kaskazini na Kati wametakiwa kuandika habari za uchunguzi zitakazochochea mabadiliko ya sera na sheria pamoja na kuhimiza uwajibikaji katika jamii.

Wito huo umetolewa wakati wa mafunzo ya waandishi wa habari za mazingira yaliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanahabari Inayosaidia Jamii za Asili (MAIPAC), yaliyofanyika jijini Arusha.

Akitoa mada katika mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya, amesema kuwa katika uandishi wa kisasa, waandishi wanapaswa kujikita zaidi kwenye habari za uchunguzi badala ya kuandika habari za matukio ya kila siku.

Amesema kuwa lengo la uandishi wa habari linapaswa kuwa kuchochea mabadiliko ya sera na sheria, lakini pia kuibua uwajibikaji kwa wadau mbalimbali.

 “Mafunzo haya yameandaliwa ili waandishi muandike habari za uchunguzi za mazingira zitakazochochea mabadiliko ya kweli huku mkizingatia maadili ya taaluma,” amesema Simbaya.

Aidha, Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma, amesema kuwa licha ya umuhimu wa kuandika habari za uchunguzi zinazobainisha changamoto katika jamii, waandishi wanapaswa kuzingatia maadili, mila na tamaduni za jamii wanazoziandikia.

Amesema waandishi wanapaswa kuandika habari zinazoonesha mapungufu katika sera, kanuni na sheria, lakini pia habari zinazoongeza ushiriki wa jamii katika kusoma, kuelewa na kushiriki katika kufanya maamuzi.

 “Habari zetu zinapaswa kuwa daraja kati ya jamii na watunga sera,” amesema Juma.

Akizungumzia uandishi wa habari kwa jamii za asili, Juma amewataka wanahabari kuheshimu mila na tamaduni zao, kuwaheshimu viongozi wa kimila na kutoandika habari bila kupata idhini ya mtu au jamii husika.

Hata hivyo, amesema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya watu kwenda kwenye maeneo ya jamii za asili kama Wahadzabe, kupiga picha na kuandika habari bila ridhaa au uelewa wa jamii hizo, hali ambayo ni kinyume na misingi ya maadili ya uandishi wa habari.

 Pia ameongeza kuwa katika kuandika habari za jamii za asili ni muhimu kutumia lugha isiyodhalilisha, kuepuka maneno yanayokera, lakini pia kuwapa fursa jamii husika kujieleza na kusimulia changamoto zao kwa sauti yao wenyewe.

Kwa upande mwingine, Juma amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo waandishi kwenda kuchunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa jamii za pembezoni, pamoja na migogoro ya ardhi ambayo imeanza kujitokeza katika maeneo mbalimbali.

Akitoa mada kuhusu ulinzi na usalama wa waandishi wa habari za mazingira, Wakili Paul Kisabo amewataka wanahabari kufanya tathmini za kiusalama kabla ya kwenda kufanya uchunguzi na kuchukua tahadhari stahiki ili kujilinda wao na vyanzo vyao vya habari.

Aidha, Wakili Kisabo ameanisha sheria mbalimbali za habari na mazingira ambazo waandishi wanapaswa kuzijua na kuzitumia ipasavyo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Mafunzo hayo yamewakutanisha waandishi wa habari 35 kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Singida, Dodoma na Manyara, yakidhaminiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

 Mafunzo kama hayo yanatarajiwa pia kufanyika katika Kanda ya Ziwa, Kanda ya Mashariki, Pwani pamoja na Zanzibar.




















Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com