
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amesema Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) ni mhimili muhimu katika kutafsiri na kutekeleza ndoto, maono na matarajio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika sekta ya uwekezaji.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Uwekezaji la Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza lililoandaliwa na TISEZA, Mhe. Kapinga alisema jukumu la Serikali na Taifa kwa ujumla ni kuwa na maono makubwa ya maendeleo, huku TISEZA ikipewa dhamana ya kuyageuza maono hayo kuwa vitendo vinavyoleta maendeleo ya kweli na endelevu kwa Watanzania.
Alieleza kuwa kupitia majukumu yake ya kuratibu, kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji nchini pamoja na kuendeleza maeneo maalum ya kiuchumi, TISEZA ni chombo muhimu katika kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Mhe. Kapinga alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi tatu bora barani Afrika katika kuvutia uwekezaji na kuwa na mazingira bora ya kufanya biashara ifikapo mwaka 2050.
Amesisitiza kuwa utekelezaji wa azma hiyo unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya TISEZA, Sekta Binafsi na Serikali kupitia mipango ya maendeleo ikiwemo MKUMBI II.






Social Plugin