Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAIMARISHA HAKI NA HUDUMA KWA WATU WASIOONA


Na Mwandishi maalum,Dodoma.

Serikali imesema inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za makusudi ili kuhakikisha watu wenye ulemavu, hususan wasioona, wanapata haki, huduma na fursa sawa na wananchi wengine katika nyanja zote za maisha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), kuelekea Maadhimisho ya Kitaifa ya Watu Wenye Ulemavu Wasioona yanayotumia maandishi ya Braille, yatakayofanyika mkoani Tanga Februari 12, Naibu Waziri Ummy Nderiananga amesema Serikali inalenga kuwawezesha watu wasioona kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.

Amesema jitihada hizo zinajumuisha utekelezaji wa sera na sheria mbalimbali ikiwemo Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (toleo la 2023), Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008, pamoja na utekelezaji wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, Sura ya 183, na kanuni za mahakama zinazohakikisha haki katika mashauri yanayohusu makundi maalumu.

Naibu Waziri Ummy ameongeza kuwa Serikali imeendelea kutoa elimu ya msingi bila malipo, kuimarisha elimu ya ufundi, kusambaza vifaa vya kujifunzia vya Braille, vitabu maalumu, pamoja na kuanzisha na kuendeleza teknolojia rafiki kwa watu wasioona ili kuongeza upatikanaji wa elimu na taarifa.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Watu Wasioona Mkoa wa Dodoma, Enock Mbawa, ameihimiza jamii ya watu wasioona na familia zinazowahudumia kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali.

Amesema kufanya hivyo kutatoa hamasa na kuipa moyo Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa Rais ndiye mbeba maono na mwenye dhamira ya dhati ya kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com