NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb), ameeleza kuridhishwa kwake na maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati mkoani Kigoma, akibainisha kuwa uwekezaji huo mkubwa unalenga kuufungua mkoa huo kiuchumi na kuimarisha usafirishaji katika Ukanda wa Maziwa Makuu.
Akizungumza Februari 19, 2026, mara baada ya kukagua miradi katika Bandari ya Kigoma na Kibirizi, Mhe. Kihenzile amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuboresha miundombinu ya bandari nchini ili kuongeza ufanisi wa huduma na kuongeza mchango wa sekta ya uchukuzi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Katika Bandari ya Kigoma, mradi unaoendelea unahusisha ujenzi wa gati la abiria lenye urefu wa mita 130 na upana wa mita 50, pamoja na barabara ya sakafu ngumu yenye urefu wa mita 500 kwa ajili ya kuingia na kutoka bandarini. Aidha, mradi huo unahusisha ujenzi wa jengo la kisasa la abiria lenye uwezo wa kuhudumia kati ya watu 200 hadi 250 kwa wakati mmoja.
Mradi huo wa abiria unafadhiliwa kwa ruzuku (grant) kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA) kwa thamani ya dola za Marekani milioni 16.9. Mpaka sasa, utekelezaji wake umefikia asilimia 9, ambapo ukikamilika unatarajiwa kurahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria, kuongeza ushindani wa bandari hiyo na kuimarisha biashara za kikanda.
Mbali na gati la abiria, Mhe. Kihenzile amekagua pia mradi wa maboresho ya sehemu ya mizigo ambao upo katika hatua za awali za makabidhiano ya eneo la kazi. Mradi huo unalenga kuongeza uwezo wa kuhudumia mizigo na kuimarisha mapato ya Serikali, huku ukitarajiwa kuvuta wawekezaji kupitisha madini kupitia Kigoma badala ya kutumia njia ya Lobito nchini Angola.
Katika hatua nyingine, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inatekeleza mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kupitia ujenzi wa Soko la Kisasa la Kibirizi na Kituo cha Polisi. Mradi huo wenye thamani ya Shilingi bilioni 6.4, utajumuisha soko lenye vibanda 250 na uwezo wa kuhudumia wafanyabiashara zaidi ya 500, lengo likiwa ni kutoa mazingira salama na yenye hadhi kwa wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi, Mha. Erick Madinda, ametoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huo wa kimkakati. Amesema maboresho hayo ni sehemu ya mpango mpana wa kuifanya Kigoma kuwa lango kuu la biashara na usafirishaji kwa nchi zinazozunguka Maziwa Makuu, jambo litakalochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Social Plugin