Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ROCK BLOCK YACHOCHEA MAPINDUZI YA UJENZI KILIMANJARO



- Ajira 122 zatengenezwa, Serikali yavuna Shilingi Milioni 400/-

📍Rombo, Februari 28, 2026

MGODI wa Rock Block uliopo Wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro, umeendelea kuwa kichocheo cha mageuzi katika Sekta ya Madini ya Ujenzi kwa kuzalisha ajira 122 na kuiingizia Serikali zaidi ya Shilingi milioni 400 katika kipindi cha miaka mitatu ya uendeshaji wake.

Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Abel Madaha, amesema hayo kupitia mahojiano maalum Wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro na kuongeza kuwa uchimbaji na uchongaji wa miamba kwa ajili ya kutengeneza matofali na bidhaa nyingine za ujenzi ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kusimamia na kuendeleza madini ya ujenzi ili kuongeza thamani na mapato ya taifa.

Amesema mgodi huo umeendelea kuchangia mapato ya Serikali kupitia ada, mrabaha na kodi mbalimbali zinazolipwa kwa taasisi ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Halmashauri ya Wilaya, hali inayochochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo la Rombo na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.

Mhandisi Madaha amefafanua kuwa miamba inayochimbwa katika eneo la Holili ilitokana na milipuko ya lava kutoka Mlima Kilimanjaro, jambo linalolifanya eneo hilo kuwa na malighafi adimu na ya kipekee inayopatikana Rombo pekee nchini.

Amesema bidhaa zinazozalishwa na mgodi huo ni pamoja na matofali ya miamba, paving blocks, vigae, coblestone, wall cladding, kerbstone zinazotumika katika utengenezaji wa kingo za barabara, pozolana — mchanga maalum mweusi unaotumika katika uzalishaji wa Saruji na kazi nyingine za ujenzi.

Kwa mujibu wa Mhandisi Madaha, matofali ya miamba yana uimara mara tatu zaidi ya matofali ya kawaida, hayaathiriwi na fangasi wala ukungu na hudumu kwa muda mrefu, jambo linaloyafanya kuwa chaguo sahihi kwa miradi ya kisasa ya ujenzi. 

Amewahimiza wawekezaji kujitokeza kuwekeza katika Sekta ya Madini ya ujenzi kwa kuwa ina fursa kubwa ya kukuza uchumi na ajira.

Naye Mkurugenzi wa Rock Block Limited, Fabian Woisso, amesema kampuni hiyo imeajiri wafanyakazi 72 wa kudumu na vibarua 50, hatua inayochangia kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana katika eneo hilo.

Amesema soko la bidhaa zao ni la ndani ya nchi, hususan katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Dodoma na Dar es Salaam, ambapo mahitaji ya vifaa vya ujenzi yamekuwa yakiongezeka kufuatia kukua kwa miradi ya miundombinu na makazi.

Aidha, Woisso amesema kampuni imewekeza katika miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR), ikiwemo ujenzi wa barabara ya kilomita tisa kutoka Holili hadi Kidondoni, ujenzi wa darasa katika Shule ya Msingi Kidondoni na uchangiaji wa matofali kwa shule na vituo vya polisi.

Amehitimisha kwa kuwataka vijana kuchangamkia fursa zilizopo katika Sekta ya Madini ya Ujenzi, akisisitiza kuwa sekta hiyo ina uwezo wa kuongeza ajira, mapato ya taifa na kuimarisha maendeleo ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.












Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com