Na Sumai Salum- Kishapu
Afisa Ustawi wa Jamii wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Mwajuma Abeid akizungumza wakati akifungua kikao cha utekelezaji wa PJT-MMMAM mwezi Oktoba-Disemba 2025, kwa niaba ya Mganga Mkuu wilayani humo chenye lengo la kupata uelewa wa kadi alama ya tathmini ya maendeleo ya awali ya Mtoto (ECD), Changamoto zilizotambuliwa na njia za kutatua changamoto hizo zinazoikabili programu hiyo Februari 19,2026
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imeendelea kutekeleza Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT–MMMAM) kwa lengo la kuhakikisha watoto wanapata malezi bora tangu wakiwa katika hatua za awali za maisha.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa programu hiyo kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025 Mratibu wa PJT–MMMAM wilayani humo,Paul Lupolaso, kwenye kikoa chenye lengo la kupata uelewa wa kadi alama ya tathmini ya maendeleo ya awali ya Mtoto (ECD), Changamoto zilizotambuliwa na njia za kutatua changamoto hizo Februari 19,2026.
Katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri imeendelea kutekeleza shughuli mbalimbali zikiwemo utoaji wa elimu ya afya na lishe kwa jamii, kampeni za kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga, jitihada za kukabiliana na udumavu, pamoja na utoaji wa elimu ya kuzuia ukatili dhidi ya watoto.
"Katika kipindi hiki tumeweza kutoa vidonge vya madini chuma kwa wanawake wajawzito na kufikia 91%, elimu ya kinamama kujifungulia vituo vya afya 90%, Watoto kunyonya maziwa ya mama pekee wenye umri wa miezi 0 mpaka miezi 6 kwa 98%" ameongeza Lupolaso
Aidha, ameongeza kuwa elimu ya usalama wa mtoto imeendelea kutolewa katika shule za msingi 128 zilizopo ndani ya Wilaya ya Kishapu. Hata hivyo, amebainisha kuwa utekelezaji wa programu hiyo umekumbana na changamoto kadhaa ikiwemo upungufu wa watumishi katika kitengo cha lishe, ushiriki mdogo wa wanaume katika masuala ya afya na lishe ya familia, pamoja na uhitaji wa kuimarisha usimamizi elekezi katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Kutokana na changamoto hizo, Halmashauri imeweka mikakati ya kuimarisha utekelezaji wake kwa kufanya kikao cha Kamati ya Lishe kwa kushirikiana na Watendaji wa Kata, kuhimiza maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe (SaLiki), kufanya usimamizi elekezi katika vituo vya afya na zahanati, kuongeza uhamasishaji wa jamii kuhusu usafi wa mazingira na umuhimu wa kinamama kujifungulia katika vituo vya afya, pamoja na kutoa mafunzo kazini kwa watoa huduma kuhusu huduma za dharura kwa mama na mtoto.
Baada ya uwasilishaji wa taarifa hiyo, wajumbe walitoa maoni mbalimbali ya kuboresha programu hiyo, wakisisitiza umuhimu wa kuongeza mikakati ya kuwahusisha wanaume katika kliniki za wajawazito na masuala ya lishe ili kuimarisha uwajibikaji wa familia, kuanzisha vikundi vya wazazi katika ngazi ya jamii vitakavyosaidia kutoa elimu ya malezi chanya, pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa takwimu sahihi zitakazosaidia katika upangaji na utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya mtoto.
Sambamba na hayo, Halmashauri pia imeendelea kutoa shukrani kwa wadau wanaoiunga mkono katika utekelezaji wa programu hiyo wakiwemo World Vision, THPS, Marie Stopes, AMREF, Kivulini na REDESO kwa mchango wao katika kuboresha ustawi wa watoto na jamii kwa ujumla.
Ikumbukwe kuwa Serikali ilizindua rasmi programu hiyo mwezi Desemba 2021 ikiwa na dhamira ya kuimarisha mfumo jumuishi wa malezi ya mtoto unaojikita katika maeneo ya afya bora, lishe, malezi yenye mwitikio, fursa za ujifunzaji wa awali pamoja na ulinzi na usalama wa mtoto.
Social Plugin