
Na Sheila Ahmadi – Dar es Salaam
Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imetenga eneo maalumu la kuhifadhia makasha (makontena) ili kuongeza ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake bandarini hapo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema hatua hiyo inalenga kupunguza msongamano na kuboresha utendaji wa bandari, hususan katika kuhudumia idadi kubwa ya makasha yanayoingia na kutoka.
Prof. Mbarawa amesema kabla ya uwekezaji wa sasa, Bandari ya Dar es Salaam kupitia Terminal namba moja na mbili ilikuwa inapokea takribani makasha 800,000 kwa mwaka. Hata hivyo, baada ya kuingia kwa mwekezaji, matarajio ni kuongeza idadi hiyo hadi kufikia makasha milioni 1.3 kwa mwaka, sawa na ongezeko la takribani asilimia 50.
Ameeleza kuwa eneo hilo jipya la kuhifadhia makasha litakuwa na uwezo wa kuhifadhi makasha 150,000 kwa wakati mmoja, na litasaidia kupunguza changamoto ya msongamano wa magari jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zikiwemo TRA, TPA na TASAC. Amesema mkandarasi anatarajiwa kukamilisha eneo hilo ifikapo mwezi Februari mwaka huu.
Kwa upande wa usafirishaji, Prof. Mbarawa amesema hapo awali bandari ilikuwa ikihudumia wastani wa makasha 200 kwa siku kupitia reli, lakini kuanzia tarehe 15 Februari, treni tano zitaanza kutoa huduma ya usafirishaji wa makasha, hatua itakayoongeza ufanisi na mapato ya bandari.
Akizungumzia mapato, amesema Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeongeza makusanyo kwa kiwango kikubwa.
Ametaja kuwa kipindi cha nyuma makusanyo yalikuwa takribani shilingi bilioni 8, huku kwa sasa yakifikia takribani shilingi trilioni 1.4, na tangu kuanza kwa ushirikiano na mwekezaji, makusanyo yamefikia shilingi trilioni 2.03.
Ameongeza kuwa sehemu ya fedha hizo, kiasi cha shilingi bilioni 550 kutoka TPA, zinaelekezwa katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa lengo la kukuza uchumi wa bandari na taifa kwa ujumla.
Pia ameainisha kuwa makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yameongezeka kutokana na uboreshaji wa utendaji bandarini.
Prof. Mbarawa ametoa wito kwa watumishi wote wa bandari kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kazi, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji katika bandari za nchini.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus, amesema maboresho ya mashine na mifumo ya kisasa yameongeza kwa kiasi kikubwa ufanisi wa bandari hiyo, hususan katika Terminal namba moja.
Amesema hapo awali meli zilikuwa zikihudumiwa kwa wastani wa siku 10 zikiwa gati, lakini kwa sasa muda huo umepungua hadi siku tatu pekee, huku upakuaji na upakiaji ukifanyika ndani ya saa 24.





























Social Plugin