Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMPENI YA MAFUNZO KWA WAJASIRIMALI WADOGO YAZINDULIWA KUELEKEA MAADHIMISHO YA WIKI YA USALAMA NA AFYA KAZINI 2026

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, akiwasilisha hotuba yake ya kufunga mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wanachama wa kikundi cha Wanawake Wachimbaji Bukombe (WAWABU).

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu,amezindua kampeni ya mafunzo kwa wajasiriamali wadogo ambayo ni sehemu ya programu za uhamasishaji masuala ya usalama na afya kazini kuelekea maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Aprili 28, 2026.

Kampeni hiyo imeanza kwa kutoa mafunzo kwa wanachama wa umoja wa Wanawake Wachimbaji Bukombe (WAWABU) wanaofanya shughuli za uchimbaji madini katika Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita ambayo yametolewa mwishoni mwa wiki (Februari 21, 2026).

Akifunga mafunzo hayo ya siku moja kwa wanawake zaidi ya 350, Waziri Sangu, mbali na kuwapongeza wakazi wa Bukombe kwa kuwa wachapakazi, amesisitiza juu ya umuhimu wa kuzingatia masuala ya usalama na afya katika shughuli za uchimbaji madini hususan kwa wachimbaji wadogo ambao mazingira yao ya kazi yana vihatarishi vingi na teknolojia yao ni duni.

“Tunafanya mafunzo haya kwa kutambua umuhimu wake kwa wachimbaji wadogo. Tumekuwa tukipata taarifa za matukio mengi ya ajali hususan kwa wachimbaji wadogo kufukiwa na vifusi wakiwa wanatekeleza majukumu yao. Hii ni kutokana na kuwa uchimbaji wenu mara nyingi hautumii teknolojia za kisasa ambazo ni ghali na upatikanaji wake ni mgumu,” amesema Waziri mwenye Dhamana ya Masuala ya Kazi na kuongeza:

“Nimefurahi sana kuonana na kundi la wachimbaji wanawake zaidi ya 350 kwani mara nyingi tumezoea kuona shughuli hizi zinafanywa na wanaume tu. Hivyo, ninawapongeza sana nasisi tutaendelea kuunga mkono jitahida zenu kwa kuwawezesha kufanya kazi kwa tija na katika hali ya usalama.”

Amemuagiza Mtendaji Mkuu Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda, kuhakikisha mpango huo wa mafunzo unakuwa endelevu na kuyafikia makundi mengi zaidi ya wachimbaji wadogo na wajasiriamali katika sekta nyingine za kiuchumi.

Aidha, Waziri Sangu, ametoa rai kwa wachimbaji wadogo kuzingatia masuala mbalimbali waliyofundishwa katika mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na matumizi endelevu ya vifaa kinga ambavyo baadhi vimetolewa na OSHA kupitia programu hiyo.

Akizungumza nje ya ukumbi wa mafunzo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi.Khadija Mwenda, amesema lengo la programu ya mafunzo kwa makundi mbalimbali ya wajasiriamali wadogo ni kuwatambua na kuwajengea uelewa wa masuala ya usalama na afya ili kuongeza kiwango cha uzingatiaji (compliance level) wa kanuni bora za usalama na afya nchini.

Aidha, ameahidi kuhakikisha kwamba mpango huo wa mafunzo unakuwa endelevu kwa mujibu wa maelekezo ya serikali yaliyotolewa na Waziri mwenye Dhamana ya Masuala ya Kazi nchini.

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Mwenyekiti wa WAWABU, Bi. Regina Kabogo, wameishukuru serikali kwa uwezeshaji waliopata wa mafunzo na vifaa kinga huku wakiiomba serikali kuwafanyia upembuzi yakinifu wa hali ya upatikanaji wa dhahabu katika vitalu 13 vinavyomilikiwa na umoja huo.

“OSHA wametufundisha vitu vingi sana kuhusiana na usalama na afya katika shughuli zetu za uchimbaji madini na wametupatia baadhi ya vifaa kinga vya muhimu jambo ambalo litatuhamasisha kufanya kazi kwa bidii ili kujiongezea kipato binafsi pamoja na mapato ya serikali,” ameeleza Bi. Regina Kabogo.

Mafunzo yalitolewa na OSHA kwa wanachama wa WAWABU yamehusisha mada mbalimbali zikiwemo dhana ya usalama na afya mahali pa kazi, vihatarishi vya usalama na afya katika sekta ya madini, sheria ya usalama na afya mahali pa kazi pamoja na misingi ya huduma ya kwanza mahali pa kazi kwa nadharia na vitendo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, akiwasilisha hotuba yake ya kufunga mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wanachama wa kikundi cha Wanawake Wachimbaji Bukombe (WAWABU).

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi.Khadija Mwenda, akitoa maelezo ya awali kuhusu mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa na Taasisi yake kwa wanachama wa kikundi cha Wanawake Wachimbaji Bukombe (WAWABU) katika haflaya kufunga mafunzo hayo.

Mwenyekiti wa kikundi cha Wanawake Wachimbaji Bukombe (WAWABU), Bi. Regina Kabogo, akiwasilisha salamu za wachimbaji hao katika hafla ya kufunga mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa kwao na OSHA ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu alikuwa Mgeni Rasmi.
Wanachama wa kikundi cha Wanawake Wachimbaji Bukombe (WAWABU), wakifuatilia nasaha na hotuba za viongozi mbalimbali katika hafla ya kufunga mafunzo ya usalamana afya mahali pa kazi yaliyotolewa kwao na OSHA ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi yaWaziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu alikuwa Mgeni Rasmi.
Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Paskas Muragili, akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mhe. Deus Sangu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) katika hafla yakufunga mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wanachama wa Umoja wa Wanawake Wachimbaji Bukombe (WAWABU).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, akikabidhi vifaa kinga na masunduku ya huduma ya kwanza kwa wanachama wa Umoja wa Wanawake Wachimbaji Bukombe (WAWABU) katika hafla ya kufunga mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa kwao na OSHA. Vifaa hivyo vilitolewa na OSHA kama sehemu ya programu yao ya mafunzo na kuhamasisha masuala ya usalama na afya miongoni mwa makundi mbalimbali ya wajasiriamali wadogo nchini.

 

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi.Khadija Mwenda, akisisitiza juu ya umuhimu wa matumizi sahihi ya vifaa kinga baada ya kukamilika zoezi la kukabidhi vifaa kinga kwa wanachama wa Umoja wa Wanawake Wachimbaji Bukombe (WAWABU) katika hafla yakufunga mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa kwao na OSHA.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu(katikati), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na washiriki wa mafunzo katika hafla ya kufunga mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wanachama wa Umoja wa Wanawake Wachimbaji Bukombe (WAWABU).

Wanachama wa Umoja wa Wanawake Wachimbaji Bukombe (WAWABU) wakimpokea kwa bashasha Mgeni Rasmi, Mhe. Deus Sangu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu(Kazi, Ajira na Mahusiano) na viongozi alioambatana nao akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Paskas Muragili na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, katika hafla ya kufunga mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wanachama waWAWABU.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com