Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HAKUNA KUPIGA MZINGA NI MDOGOMDOGO MPAKA KINAELEWEKA


Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imezidi kudhihirisha kuwa "haipigi mizinga" wala kutoa ahadi hewa, bali inatekeleza kwa vitendo mikakati ya kuimarisha wachimbaji wadogo nchini.

Katika hafla ya kihistoria iliyofanyika Februari 23, 2026, katika Hoteli ya Johari Rotana, Benki ya CRDB na Tume ya Madini zimetia saini makubaliano yatakayobadili kabisa sura ya uchimbaji mdogo wa dhahabu nchini Tanzania.

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesisitiza kuwa dhamira ya Rais Samia ni kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo ili watoke kwenye uchimbaji wa kubahatisha na kuingia kwenye uchimbaji wa kisayansi na tija. 

"Hatua hii ni sehemu ya mfumo wetu madhubuti wa usimamizi na kutoa leseni katika maeneo yaliyokuwa yamelala kwa muda mrefu," alisema Mavunde. Alibainisha kuwa sekta hii tayari imetoa ajira kwa zaidi ya watu 18,000, na lengo ni kuongeza idadi hiyo kupitia uwezeshaji wa mitaji.

Ili kuhakikisha mchimbaji mdogo hapotezi gharama kwa kuchimba pasipo na madini, Serikali imejipanga kufikia asilimia 50 ya utafiti wa kina wa kijiolojia ifikapo mwaka 2030. 

Waziri Mavunde alitangaza habari njema kuwa Tanzania iko katika hatua za mwisho za ununuzi wa helikopta maalumu kwa ajili ya tafiti za angani. Helikopta hizi zitasaidia kupata takwimu sahihi za miamba migumu na kupunguza gharama za utafiti, jambo ambalo limekuwa mwiba kwa wachimbaji wadogo kwa miaka mingi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, ameweka wazi kuwa benki hiyo tayari imeshatoa jumla ya shilingi bilioni 189 kusaidia sekta ya madini. 

Alisisitiza kuwa wachimbaji wadogo si "wadogo" kwa mchango wao, bali ni nguzo muhimu ya uchumi wa taifa. Mpango huu mpya unalenga kutoa mikopo nafuu na yenye masharti wezeshi ili kuwawezesha wachimbaji kununua vifaa vya kisasa na kuongeza thamani ya dhahabu yao hapa hapa nchini.

Ushirikiano huu kati ya Serikali kupitia Tume ya Madini na sekta binafsi kupitia Benki ya CRDB, ni matokeo ya usimamizi mzuri wa Wizara ya Madini chini ya maelekezo ya Rais Samia.

Lengo ni kuhakikisha sekta ya madini inakuwa kichocheo kikuu cha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ikipunguza umaskini na kuimarisha mapato ya ndani bila kutegemea misaada ya nje, bali kwa kutumia rasilimali zetu wenyewe mdogomdogo kuelekea mafanikio makubwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com