Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo Akizungumza wakati wa semina ya wahariri iliyoandaliwa na FCC jijini Dar es Salaam.Na Mwandishi Wetu - Dar es salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema ataimarisha ushirikiano kati ya ofisi yake na Tume ya Ushindani (FCC) katika mapambano dhidi ya bidhaa bandia na viwanda bubu ndani ya Jiji la Dar es Salaam. Amesema hatua kali zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kuvuruga uchumi wa soko.
Amesema hayo wakati wa semina ya wahariri iliyoandaliwa na FCC jijini Dar es Salaam, akisisitiza kuwa ofisi yake kwa kushirikiana na halmashauri zote itaongeza udhibiti wa uzalishaji na biashara. Amesema lengo ni kuwabaini na kuwachukulia hatua wanaojihusisha na usambazaji wa bidhaa zisizo halali.
Amesema kumekuwepo na ongezeko la viwanda bubu vinavyozalisha bidhaa feki, hali inayochangia kuvuruga ushindani wa soko, kupunguza mapato ya Serikali na kuhatarisha afya za wananchi. Amesema Ilala ni lango la biashara, hivyo usimamizi wake unapaswa kuwa makini zaidi.
Aidha, amesema FCC inapaswa kuongeza idadi ya watumishi kutokana na majukumu yake kuwa makubwa, hususan katika mipaka na bandarini. Amesema kuongezeka kwa shehena katika Bandari ya Dar es Salaam kunahitaji nguvu kazi ya kutosha kudhibiti bidhaa zinazoingia nchini.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, akizungumza na wahariri wakati wa semina ya wahaririKwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, amesema taasisi hiyo inaendelea kutekeleza maono ya Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mazingira ya ushindani na kuvutia wawekezaji. Amesema sheria ya ushindani ni kigezo muhimu kwa mwekezaji kabla ya kuamua kuwekeza.
Amesema semina hiyo imelenga kuwajengea uwezo wahariri kuhusu Sheria ya Ushindani ya mwaka 2003 na mabadiliko yanayotarajiwa kupelekwa bungeni. Amesema FCC haiko tayari kuona soko linapangwa kwa namna inayowaumiza wananchi.
Naye Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bakari Kimwanga, amesema ushirikiano kati ya FCC na wahariri ni muhimu katika kutoa elimu kwa umma. Amesema hatua hiyo itasaidia kulinda ushindani wa soko na maslahi ya watumiaji nchini.


.jpg)



Social Plugin