
Mkandarasi huyo, aliyesaini mkataba tangu mwaka 2022 kwa barabara ya kilometa 15.2, amejenga kilometa moja pekee ndani ya muda wa nyongeza.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kabetu, mbele ya Baraza la Madiwani, ameweka wazi kuwa Serikali haina muda wa kulea wazembe.
"Tumekatisha mkataba. Hatuwezi kusubiri muujiza wakati wananchi wanahitaji barabara kufika hospitali na masokoni," alisema Kabetu akijibu hoja ya Diwani wa Viti Maalumu, Herietha Makaga.
Uamuzi huu wa Kahama ni kielelezo cha namna Tanzania inavyojipanga kuelekea mwaka 2050. Dira hiyo inasisitiza kuwapo kwa miundombinu imara kwani barabara si pambo, ni mshipa wa uchumi.Aidha kwa wananchi wanapopata huduma (barabara, stendi, masoko), amani inatawala. Chuki huzaliwa pale miradi inapokwama na mashimo yanapozuia wagonjwa kufika hospitali.
Wakazi wa Kahama, Kulwa Jumanne na Sophia Kalebo, wamepongeza hatua hiyo wakisema barabara hiyo ilikuwa "mtego wa ajali". Walisisitiza kuwa wananchi hawahitaji siasa, wanahitaji miundombinu itakayowasaidia kukuza vipato vyao.
Serikali imetangaza kuwa ndani ya miezi miwili, mkandarasi mpya mwenye kasi atakuwa kazini. Huu ni mchoro mpya wa uongozi: Haki, Uwajibikaji, na Maendeleo kwanza!
Social Plugin