Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ACHENI KUBEZA UWEKEZAJI WA WAZAWA, NI NGUZO YA MAENDELEO NA AFYA YA JAMII


SERIKALI imewataka wananchi kote nchini kuacha tabia ya kubeza na badala yake kuanza kuwathamini na kuwakumbatia wawekezaji wazawa, ikielezwa kuwa wao ni nguzo muhimu katika kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo yao.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Dkt. Jafar Seif, alipofanya ziara ya kikazi mkoani Geita kukagua shughuli za maendeleo, ikiwemo uwekezaji unaofanywa na wazalendo katika sekta ya madini.

Akizungumza baada ya kutembelea mgodi wa mwekezaji mzawa, King Mapung’o uliopo mkoani hapa, Dkt. Seif alisema kuwa uwekezaji wa ndani una faida kubwa ya kipekee kwani fedha zinazopatikana hubaki ndani ya nchi na kusaidia ujenzi wa miundombinu ya huduma za kijamii.

“Tunaposema tuthamini wawekezaji wazawa, tunamaanisha hawa ndio watu ambao wanaguswa moja kwa moja na matatizo ya wananchi wenzetu. Wanapopata faida, hawaipeleki nje ya nchi, bali wanashirikiana na Serikali kujenga shule, zahanati na barabara katika maeneo yenu,” alisema Dkt. Seif.

Katika kuonyesha mfano wa kivitendo wa namna mwekezaji mzawa anavyoweza kuisaidia serikali, mwekezaji huyo, King Mapung’o, ametangaza kutoa ufadhili wa Bima ya Afya kwa wananchi 600 wa mkoani Geita.

Hatua hiyo imetajwa na Dkt. Seif kuwa ni muendelezo wa kuunga mkono maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa akipigania Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata matibabu bila vikwazo vya kifedha.

“Huu ni mfano wa kuigwa. Kitendo cha mwekezaji mmoja kulipia bima ya afya watu 600 ni mzigo mkubwa alioutua serikali na ni msaada mkubwa kwa wananchi hawa ambao sasa watapata matibabu bora bila hofu ya gharama. Huu ndio uzalendo tunaoutaka,” alisisitiza Naibu Waziri huyo.

Dkt. Seif alibainisha kuwa kuwekeza kwa wazawa kuna faida nyingi, ikiwemo ajira kwa vijana,uhamisho wa ujuzi na utulivu wa kiuchumi.

Aidha, Naibu Waziri huyo aliwaasa watendaji wa serikali katika ngazi za mitaa kuacha kuweka vikwazo visivyo na tija kwa wawekezaji wazawa, badala yake wawape ushirikiano wa karibu ili waweze kukua na kutoa mchango mkubwa zaidi.

Kwa upande wake, mwekezaji King Mapung’o aliahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika kila hatua, akisisitiza kuwa jukumu la kuijenga Tanzania si la serikali pekee, bali ni la kila mdau anayenufaika na rasilimali za nchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com