Na Marco Maduhu, SHINYANGA
MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa, amempongeza Naibu Waziri wa Nishati Salome Makamba anayetokana na UWT, kwa kutopandisha mabega kulingana na nafasi yake, na kuhudhuria kikao cha Baraza cha Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) CCM Mkoani humo, licha ya kuwa na vikao vingi pamoja na kuhitajika Jijini Mwanza kwenye mambo mengine, lakini ametanguliza chama kwanza.
Mabala ametoa pongezi hizo leo Februari 20, 2026, wakati akifungua kikao cha baraza cha UWT, CCM mkoani humo.
Amesema, amefarijika kumuona Naibu Waziri wa Nishati Salome Makamba kwenye kikao hicho, pamoja na Mjumbe wa Mkutano wa SADC Mwanahamisi Munkunda, kwa kutanguliza Chama kwanza licha ya kuwa na vikao vingi, na kusema kwamba huo ndiyo uzalendo.
“Nakupongeza Naibu Waziri wa Nishati Salome Makamba kwa kuhudhuria kikao hiki cha baraza la UWT pamoja na mwenzako Mjumbe wa SADC Mwanahamisi, kutokana na nafasi zenu mngeweza kupandisha mabega na kutohudhuria kabisa na kutoa udhuru kuwa mnavikao vingi, lakini kwa uzalendo wenu mmetanguliza chama kwanza,” amesema Mabala.
“Najua Salome una mkutano mwingine Mwanza na ulipaswa kuwepo huko, lakini kukasema uhudhurie kwanza kwenye kikao hiki cha UWT hapa Shinyanga, nafasi yako uliyonayo upo kwa ajili ya kumsaidia Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, na wanawake wa Shinyanga, hongera sana kwa kuaminiwa na Rais na kuonyesha uzalendo,” ameongeza.
Aidha, amemwagia pia sifa Salome Makamba, kwamba yeye siyo mtu wa maneno maneno wala kuwa na makundi, bali ni mtu wa kuchapa kazi na kutekeleza maagizo ambayo hupewa, na kumsihi aendelee hivyo hivyo kukitumikia Chama na Taifa kwa ujumla kwa kuwaletea maendeleo wananchi kupitia Sekta ya Nishati.
Katika hatua nyingine Mabala amewaomba UWT Mkoani humo waendelee kuwa na umoja, mshikamano na upendo na kujiepusha na migogoro ili kuendeleza Jumuiya yao ipate kusongambele, na kuimarika zaidi.
Naye Naibu Waziri wa Nishati Salome Makamba, akizungumza kwenye kikao hicho, amesema amefarijika kuhudhuria kikao hicho, huku akiwashukuru UWT kwa kumpigia kura nyingi za ushindi Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, pamoja na kumshukuru Rais kwa kumuamini na kumpatia dhamana ya kuwa Naibu Waziri wa Nishati, kwamba ataitendea haki nafasi hiyo kwa kuchapa kazi, na hatowaangusha wanawake wa Shinyanga.
“Kwa mara ya kwanza UWT Mkoa wa Shinyanga umetoa Naibu Waziri wa Nishati kupitia Vitimaalum, hii dhamana ambayo nimepewa na Rais ni kubwa sana, sitowaangusha wanawake wa Shinyanga nitachapa kazi kwa bidii zote kumsaidia Rais,” amesema Makamba.
TAZAMA PICHA👇👇
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa akizungumza.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Shinyanga Grace Bizulu akizungumza.
Naibu Waziri wa Nishati Salome Makamba akizungumza.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa (kulia) akimpatia Cheti cha Pongeza Naibu Waziri wa Nishati Salome Makamba, ambaye pia ni Mbunge wa Vitimaalum Mkoa wa Shinyanga.
Social Plugin