Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI WA ULINZI APONGEZA JWTZ KWA KASI YA UJENZI MAKAO MAKUU YA ULINZI NA HOSPITALI YA MSALATO


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Rhimo Simeon Nyansaho, amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa hatua kubwa iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi miwili ya kimkakati jijini Dodoma.

Miradi hiyo ni ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa (MMUT) yaliyopo Kikombo, pamoja na Hospitali Kuu ya Rufaa ya Jeshi iliyopo Msalato.

Mhe. Nyansaho alitoa pongezi hizo alipokuwa akizungumza na makamanda pamoja na wapiganaji wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya miradi hiyo.

Katika ziara hiyo, Waziri Nyansaho alipokelewa na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Luteni Jenerali Salum Haji Othman.

Akiwa MMUT Kikombo, Waziri alipokea taarifa ya maendeleo ya mradi huo ambao ujenzi wake ulianza rasmi mwaka 2020, ikiwa ni sehemu ya mpango wa serikali kuhamishia shughuli zote za kimkakati jijini Dodoma.

Baada ya ukaguzi huo, Waziri alielekea Msalato kukagua ujenzi wa Hospitali Kuu ya Rufaa ya Kijeshi. Mhe. Nyansaho alielezea kufurahishwa kwake na viwango vya ujenzi na kusisitiza kuwa kukamilika kwa hospitali hiyo kutaongeza nguvu katika utoaji wa huduma za afya za kiwango cha juu jijini Dodoma.

"Kukamilika kwa hospitali hii kutahakikisha upatikanaji wa huduma bora na za kisasa za matibabu, jambo ambalo ni muhimu sana kwa askari wetu na wakazi wa jiji la Dodoma kwa ujumla," alisisitiza Mhe. Nyansaho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com