Dodoma
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, amekutana na uongozi wa Chama cha Mabroka wa Madini Tanzania (CHAMMATA) jijini Dodoma kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili mabroka wa madini nchini.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, pamoja na watendaji wengine kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini, hatua inayoonesha dhamira ya Serikali kushirikiana kwa karibu na wadau wa sekta ya madini katika kuendeleza sekta hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wanachama wa CHAMMATA, Mwenyekiti wa chama hicho, Jeremia Kituyo, amewasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili mabroka wa madini, ambapo mara baada ya kusikiliza hoja na maoni yaliyowasilishwa, Naibu Katibu Mkuu Mbibo amewahakikishia viongozi wa CHAMMATA kuwa Serikali itayafanyia kazi mapendekezo hayo kwa kushirikiana na taasisi husika, ili kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Mbibo amesisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wadau wote wa sekta ya madini, wakiwemo wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini, wanafanya kazi katika mazingira rafiki, salama na yenye tija kwa maendeleo ya sekta hiyo.
Ameongeza kuwa jitihada hizo zinalenga kuongeza uzalishaji, kuimarisha biashara ya madini kwa uwazi na ushindani, pamoja na kuhakikisha mchango wa sekta ya madini unaendelea kukua na kuchangia ipasavyo katika Pato la Taifa na maendeleo ya uchumi wa nchi kwa ujumla.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau wa sekta ya madini wameipongeza Wizara ya Madini kwa kuchukua hatua kubwa za kuwawezesha wananchi, ikiwemo utoaji wa leseni za madini kwa vikundi vya vijana, kuwarasimisha wadau wa madini na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za madini kwa mujibu wa sheria na kanuni za madini.
Aidha, wadau hao wameiomba Wizara ya Madini kuendelea kutoa msaada zaidi, hususan katika kuwaunganisha na Taasisi za Fedha ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo itakayowaongezea uwezo wa mitaji na kuchochea ukuaji wa biashara zao za madini nchini.





Social Plugin