Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAGEUZI MAKUBWA YA MIUNDOMBINU YA MAFUTA NA GATI: TANZANIA KUJENGA GATI NA MATANGI 15 YA KISASA



Na Beda Msimbe, BSKY Media

Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika leo Januari 20 kwenye Bandari ya Dar es Salaam, Msemaji Mkuu wa Serikali Ndugu Gerson Msigwa amebainisha hatua kubwa zinazochukuliwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) katika kuimarisha uwezo wa nchi kuhifadhi nishati.

Mradi mmoja wapo wa kimkakati uliotajwa ni ujenzi wa gati maalum na matangi 15 ya kuhifadhia mafuta (Tank Farms). Mradi huu una uwezo mkubwa wa kupokea na kuhifadhi mafuta hadi lita 378,000 kwa wakati mmoja, na utekelezaji wake kwa upande wa ujenzi wa matanki na miundombinu ya kupokelea mafuta (Single Receiving Terminal - SRT) umeshafikia asilimia 35.

Kukamilika kwa mradi huu kutaongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam katika kuhudumia meli za mafuta, kupunguza gharama za upakuaji, na kuhakikisha usalama wa nishati nchini.

Aidha, Msigwa ameweka wazi kuwa maboresho ya gati namba 8 hadi 11 yapo katika hatua ya manunuzi ya mkandarasi, huku upembuzi yakinifu wa ujenzi wa gati namba 12 hadi 15 ukiwa umekamilika katika awamu yake ya kwanza.

Amesema Serikali kwa sasa inatafuta wabia wa kutekeleza mradi huo wa gati namba 12-15 ambao utakuwa na tija kubwa katika kuongeza uwezo wa bandari kuhudumia shehena ya makasha. Sambamba na hayo, mradi wa uboreshaji wa gati la Malindi (Malindi Wharf) wenye urefu wa mita 500 umeshafikia asilimia 8 ya utekelezaji, jambo litakalowezesha kupokelewa kwa meli mbili kubwa zenye uzito wa tani 50,000 kila moja kwa wakati mmoja.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com