Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HALI YA BARABARA CHINYOYO YAWATESA WANANCHI




Na Barnabas Kisengi , Dodoma

Wananchi wa Mtaa wa Chinyoyo, Kata ya Kilimani Jijini Dodoma, wameiambia Gazeti la Mwananchi kuwa wanaishi katika mazingira magumu kutokana na miundombinu mibovu ya barabara, ambazo katika kipindi cha masika huwa hazipitiki kabisa, hali inayohatarisha usalama, afya na kuathiri kwa kiasi kikubwa shughuli zao za kila siku.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wamesema kila mvua inapo nyesha, shughuli za kiuchumi husimama ghafla kutokana na barabara kujaa maji, matope na mashimo makubwa, hali inayowalazimu baadhi yao kusitisha safari, watoto kushindwa kufika shule kwa wakati, na wagonjwa kushindwa kuwahi huduma za afya.

“Unakuta mgonjwa ana hali mbaya lakini gari haliwezi kupita,tunabeba wagonjwa kwa mikono au pikipiki kwa shida sana, "amesema na kuongeza;

Hii ni hatari kwa maisha yetu,tunaomba msaada wa serikali kurekebisha miundombinu hii ili tufanye kazi bila vikwazo, ” amesema Haruna Samson mmoja wa wakazi wa mtaa huo.

Kutokana na hayo Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Dodoma Mjini, Mhandisi Emmanuel Mfinanga, ameahidi kuchukua hatua za haraka kwa kuwatuma wataalamu wa TARURA kukagua barabara hizo ndani ya siku mbili.

Mhandisi Mfinanga ametoa kauli hiyo Januari 21, 2026, alipokuwa akizungumza na Diwani wa Kata ya Kilimani, Mussa Mkunda, katika ofisi za TARURA Jijini Dodoma.

“Barabara za Mtaa wa Chinyoyo ninazifahamu vizuri na changamoto zake nazijua. Changamoto kubwa ni upana mdogo wa barabara nyingi ambao uko chini ya mita nne, jambo linalofanya hata kuingiza mitambo ya ujenzi kuwa vigumu,” amesema.

Hata hivyo, amesema licha ya changamoto hiyo, TARURA iko tayari kushirikiana na uongozi wa kata na wataalamu wake ili kutafuta suluhisho la haraka na la kudumu.

“Nakuhakikishia Diwani, ndani ya siku mbili nitapita na wataalamu wangu ili tuzitembelee barabara hizo na kujadiliana kwa pamoja namna bora ya kuziboresha, ili wananchi waweze kuzitumia bila adha,” amesisitiza Mhandisi Mfinanga.

Aidha, amesema changamoto ya miundombinu ya barabara imeikumba kata nyingi kati ya Kata 41 za Wilaya ya Dodoma Mjini, lakini Mtaa wa Chinyoyo ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi kutokana na msongamano mkubwa wa watu na miundombinu isiyokidhi mahitaji ya sasa.

“Ni lazima tukae pamoja, viongozi na wataalamu, tushirikiane kutafuta suluhisho la kudumu,lengo letu ni kuondoa adha kwa wananchi na kurejesha matumaini yao,” ameongeza Meneja huyo wa TARURA.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kilimani, Mussa Mkunda, amesema Mtaa wa Chinyoyo ndio unaompa changamoto kubwa zaidi, kiasi cha kumkosesha usingizi kutokana na malalamiko ya kila siku kutoka kwa wananchi.

“Katika mitaa yote ya kata yangu, Mtaa wa Chinyoyo ndio unanipa presha kubwa zaidi. Kila mvua ikinyesha, wananchi wanapishana nyumbani kwangu kulalamika. Barabara ni kero kubwa sana, naomba TARURA iniangalie kwa jicho la tatu ili tupate ufumbuzi wa haraka,” amesema Mkunda.

Ameongeza kuwa uharibifu wa barabara hizo unasababisha maji ya mvua kutoka maeneo ya juu kuelekea mitaa jirani ya Nyerere na Kilimani, hali inayosababisha mafuriko yanayoingia kwenye makazi ya watu na kuharibu mali zao, jambo linaloongeza hasara kwa wananchi.

Kwa upande mwingine, jitihada hizi zinaendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo imeendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika uboreshaji wa miundombinu ya barabara nchini, kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mazungumzo kati ya TARURA na uongozi wa Kata ya Kilimani yameibua mwanga wa matumaini kwa wakazi wa Mtaa wa Chinyoyo, ambao sasa wanasubiri kuona ahadi hizo zikitekelezwa kwa vitendo ili kuondoa adha waliyoishi nayo kwa muda mrefu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com