Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WIZARA YA MADINI YAONESHA UZALENDO KUPITIA MICHEZO, YAHAMASISHA AMANI NA USHIRIKI WA UCHAGUZI MKUU



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

KATIKA kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba, Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini, STAMICO na taasisi nyingine zilizo chini yake, wameandaa bonanza la michezo lililolenga kuhamasisha ushiriki wa wananchi na watumishi wake katika zoezi hilo muhimu kwa mustakabali wa taifa.

Akizungumza katika bonanza hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kuchagua viongozi bora, wenye dira ya kuleta maendeleo.

“Vyama vyote vya siasa vimefanya kampeni zao tunapaswa kuangalia sera nzuri, kuchagua viongozi bora na kuwahamasisha hata walioko majumbani kujitokeza kupiga kura. Huu ni wajibu wa kizalendo,” amesema Mhandisi Samamba.

Ameeleza kuwa bonanza hilo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha afya na mshikamano miongoni mwa watumishi wa wizara na taasisi zake, huku likiwa jukwaa pia la kueneza ujumbe wa amani na mshikamano kuelekea uchaguzi.

“Kupitia mabonanza haya tunapambana na changamoto za kiafya kama kisukari na shinikizo la damu, ambazo hutokana na kutofanya mazoezi kwa sababu ya mwingiliano wa kazi,” ameongeza.

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janeth Lekashingo, alibainisha kuwa bonanza hilo halikuwa la michezo tu, bali limekuwa jukwaa la kuimarisha afya ya akili, mahusiano kazini, na kuchochea morali ya kazi.

“Bonanza hili limetufanya tuwe wamoja zaidi, tushirikiane kama timu moja. Tunawashukuru viongozi wa wizara kwa kuliona hilo,” amesema Dkt. Lekashingo.

Mtakimu wa Tume ya Madini, Azihar Kashakara, aliishukuru Wizara kwa kuandaa bonanza hilo na kueleza kuwa limekuwa na faida kubwa kwa watumishi kujijenga kiafya, kukuza mahusiano na kuongeza ari ya kazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa Wizara ya Madini, Ashura Urasa, aliwataka watumishi wote wa sekta ya madini pamoja na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba kupiga kura kwa amani na kuchagua viongozi bora wa kuiongoza nchi kwa kipindi kijacho cha miaka mitano.

Bonanza hilo lilijumuisha michezo mbalimbali kama mpira wa miguu, netiboli, mbio za mita 100, mbio za magunia, kukimbia na mayai kwenye vijiko, mbio za kuku, na kuvuta kamba. Timu kutoka taasisi zote zimeshiriki na zawadi kutolewa kwa washindi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com