Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimetoa wito kwa walimu kote nchini kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, sambamba na kutumia nafasi yao muhimu katika jamii kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki zoezi hilo la kidemokrasia.
Wito huo umetolewa na Rais wa CWT, Dkt. Selemani Ikomba, wakati wa Mkutano wa Ujirani Mwema wa viongozi wa CWT kutoka Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Kati uliofanyika hivi karibuni.
Dkt. Ikomba amesema walimu ni nguzo muhimu si tu katika elimu, bali pia kama viongozi wa fikra na maadili ndani ya jamii, hivyo wana wajibu wa kuhamasisha ushiriki hai wa wananchi katika masuala ya kiraia kama uchaguzi.
“Uchaguzi ni njia ya amani na kidemokrasia ya kuchagua viongozi watakaowakilisha matakwa ya wananchi na kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu,” amesema Dkt. Ikomba.
Ameeleza kuwa ushiriki wa walimu katika uchaguzi unaweza kuchangia katika kutatua changamoto zinazowakabili katika sekta ya elimu kama uhaba wa miundombinu, maslahi duni na mazingira magumu ya kufundishia.
Aidha, amewataka walimu kutumia nafasi zao kuelimisha wanafunzi, wazazi na jamii kwa ujumla kuhusu haki na wajibu wao wa kikatiba kushiriki katika uchaguzi, huku wakihimiza amani, mshikamano na uzalendo katika kipindi hiki muhimu kwa taifa.
Dkt. Ikomba pia ametoa wito kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wadau wengine kuhakikisha mazingira ya uchaguzi yanabaki kuwa salama, huru na yenye haki ili wananchi washiriki bila woga wala vikwazo.
Kwa ujumla, CWT inasisitiza kuwa ushiriki wa walimu katika mchakato wa uchaguzi ni wajibu wa kitaaluma na kijamii unaochangia kuimarisha demokrasia, utawala bora na maendeleo endelevu ya taifa.

Social Plugin