Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIONGOZI WA DINI KANDA YA KATI WATOA WITO WA TAIFA KUDUMISHA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Viongozi wa dini kutoka Kanda ya Kati wameungana kutoa wito wa kitaifa kwa Watanzania wote kuhakikisha amani na utulivu vinatawala katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Wakizungumza leo jijini Dodoma katika kongamano la viongozi wa dini kutoka mikoa ya Singida na Dodoma, viongozi hao wamesema ni jukumu la kila raia kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, kwa kuwa utulivu wa Taifa ndio nguzo kuu ya maendeleo na umoja wa kitaifa.

Askofu Evance Chande wa Kanisa la Carmel Assemblies of God alisema vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda amani kwa matendo na kauli zao, akisisitiza kwamba uchaguzi haupaswi kugawa Watanzania bali kuwaweka pamoja katika misingi ya demokrasia na umoja.

“Tunapaswa kuikumbatia amani kama tunavyokumbatia imani zetu. Uchaguzi ukipita, Tanzania inabaki kuwa moja, hivyo tusikubali kugawanywa kwa misingi ya kisiasa,”
Askofu Evance Chande

Kwa upande wake, Sheikh Mustapha Rajab, Sheikh wa Mkoa wa Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Kanda ya Kati, ambaye alikuwa mgeni rasmi wa kongamano hilo, aliwahimiza wananchi kutii mamlaka na kufuata maelekezo ya Serikali pamoja na viongozi wa dini.

“Amani si jambo la bahati mbaya, ni matokeo ya utii na hekima. Tukitii viongozi wetu na kuheshimu sheria, Taifa litaendelea kubaki salama,” Sheikh Mustapha Rajab

Kongamano hilo lililolenga kuliombea Taifa amani na utulivu kuelekea uchaguzi, lilibeba kaulimbiu isemayo:
 “Kupiga kura ni haki ya kila Mtanzania, amani na utulivu ni jukumu letu.

Viongozi hao walisisitiza kuwa jukumu la kulinda amani si la Serikali pekee bali ni la kila raia, wakihimiza Watanzania kuendeleza maombi, maelewano na uvumilivu katika kipindi chote cha uchaguzi.

Walisema amani ni urithi muhimu wa kizazi hiki kwa vizazi vijavyo, na kuwataka Watanzania wote kuwa walinzi wa amani hiyo kama ishara ya uzalendo na mshikamano wa kweli wa kitaifa.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com