Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TUNALAANI WOTE WANAOHAMASISHA MAANDAMANO – MALAIGWANAN KILIMANJARO



Na Mwandishi wetu, Kilimanjaro

Viongozi wa jamii ya Kimasai nchini Tanzania, maarufu kama Malaigwanan, wametoa tamko lao rasmi la kulaani vikali watu wanaohamasisha maandamano kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, wakisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa.

Tamko hilo limetolewa katika eneo la Donyomorwak, Wilaya ya Siha, Mkoa wa Kilimanjaro wakati wa mkutano wao wa kawaida wa Orkiama, ambapo Katibu wa Malaigwanani Tanzania, Bw. Jeremia Laizer, alisoma tamko hilo kwa niaba ya viongozi wa jamii hiyo.

Bw. Laizer amesema kuwa Malaigwanani wanaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kulinda amani na ustawi wa Taifa, huku wakihimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa utulivu na heshima siku ya uchaguzi.

“Tunawahimiza wananchi wote kudumisha amani, mshikamano na utulivu kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa zima. Tukatae uchochezi, migawanyiko na fitina. Tuchague maendeleo, umoja na mustakabali mwema wa vizazi vijavyo. Tanzania kwanza, amani kwanza,” amesema Bw. Laizer.

Kwa upande wake, mgeni rasmi wa mkutano huo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Namelok Sokoine, amepongeza msimamo wa Malaigwanani kwa kuonesha uzalendo na hekima katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Amesema kuwa jamii hiyo ni mfano wa kuigwa kwa kuunga mkono juhudi za kulinda amani na utulivu, akiwataka wananchi wa maeneo yote nchini kujitokeza kupiga kura ifikapo Jumatano, Oktoba 29, 2025, bila hofu wala uchochezi.

Aidha, baadhi ya viongozi wengine wa jamii hiyo wameahidi kuwa mabalozi wa amani katika maeneo yao, wakionya kuwa maandamano yasiyofuata taratibu mara zote huishia katika uharibifu wa mali na uvunjifu wa amani, ambapo waathirika wakubwa huwa ni wanawake, watoto na wazee.











Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com