
Jumuiya ya Maridhiano ya Mkoa wa Shinyanga imewasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura ifikapo Oktoba
29 mwaka huu, wakisisitiza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kutimiza haki ya
kikatiba ya kuchagua viongozi bora watakaowaletea maendeleo kuanzia ngazi ya
kata.
Tamko hilo limetolewa leo Oktaba 18, 2025 na Jumuiya ya Maridhiano ya Mkoa wa Shinyanga inayojumuisha
viongozi wa dini zote, viongozi wa kimila pamoja na wadau wa amani kutoka wilaya tatu za mkoa huo.
Wakizungumza kwa pamoja,
viongozi hao wamesema wataendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika
kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi kwa amani na utulivu, huku wakibainisha
kuwa uchaguzi ni tukio muhimu linalopaswa kuendeshwa kwa upendo, mshikamano na
heshima kwa kila mtu bila migawanyiko ya kisiasa.
Akisoma tamko la
viongozi hao, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Maridhiano Mkoa wa Shinyanga, ambaye pia ni Askofu Mstaafu wa Kanisa la KKKT, Emmanuel Makala, amesema kila Mtanzania ana jukumu la
kulinda amani, kwani amani ndiyo tunu na msingi wa maendeleo.
“Bila amani hakuna
maendeleo. Ni wajibu wa kila raia kuhakikisha nchi inabaki salama kabla, wakati
na baada ya uchaguzi,” amesema Askofu Makala.
Kwa upande wake, Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu, amewasihi viongozi wa dini, machifu na wazee wa mila
kuendelea kuliombea taifa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, ili Mungu
aendelee kulibariki na kuliongoza Tanzania katika umoja na utulivu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni
Mhita, amewahakikishia
wananchi kuwa maandalizi ya uchaguzi yamekamilika na kwamba siku ya kupiga kura
itakuwa salama, huku vyombo vya ulinzi na usalama vikiwa tayari kuhakikisha
kila mwananchi anatekeleza haki yake ya kidemokrasia bila hofu.
“Vyombo vya ulinzi na
usalama pamoja na tume huru ya uchaguzi vimejipanga kuhakikisha kila mmoja anapiga kura kwa amani na utulivu, na kutimiza haki yake ya msingi iliyowekwa kwa mujibu wa katiba.
Tujitokeze kwa wingi, tuwe watulivu na tuheshimu sheria,” amesema Mhita.
Viongozi hao wa dini wamehitimisha kwa kutoa wito wa kudumisha umoja, uvumilivu na maombi kwa taifa, wakisisitiza kuwa amani ndiyo silaha kubwa ya kulinda maendeleo yaliyopatikana nchini.










Social Plugin