Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SASA NI ZAMU YA SEKTA BINAFSI; SERIKALI YAPANDISHA KIMA CHA CHINI CHA MISHAHARA KWA SEKTA BINAFSI



Dar es Salaam, 

📍17 Oktoba, 2025

🆕Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, ametangaza rasmi kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeidhinisha ongezeko la *kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi kwa asilimia  33.4, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya miaka mitatu ya mapitio ya mishahara. Ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa NSSF Benjamini Mkapa Tower jijini Dar es Salaam tarehe 17 Octoba, 2025.

Mhe. Ridhiwani amesema kuwa kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi kimeongezeka kutoka Shilingi 275,060 mwaka 2022 hadi kufikia Shilingi 358,322 mwaka 2025. “Kwa mujibu wa Sheria za Kazi nchini, zoezi hili hufanyika kila baada ya miaka mitatu. Serikali imesikia kilio cha wafanyakazi na imeona ni haki kuongeza mshahara kwa kiwango cha kuridhisha, huku ikizingatia hali ya uchumi wa taifa na ustawi wa wananchi wake,” alisema.

Ongezeko hili linafuatia hatua kama hiyo iliyochukuliwa kwa watumishi wa umma, ambapo Serikali ilipandisha mishahara kwa asilimia 35.1,  na kufanikisha kima cha chini cha mshahara kuwa Shilingi 500,000, kama ilivyotangazwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi).

Amefafanua kuwa hatua hizi mbili kwa sekta ya umma na binafsi zinaashiria juhudi za makusudi za Serikali katika kuboresha maisha ya wafanyakazi na kuongeza tija katika maeneo ya uzalishaji, huduma, na ujenzi wa uchumi wa taifa. “Sasa ni zamu ya sekta binafsi. Serikali inaamini kuwa sekta binafsi ni injini ya uchumi. Kwa hiyo, ustawi wa wafanyakazi wake ni jambo la lazima,” 

Aidha amesema kuwa kupandishwa kwa kima cha chini cha mshahara kunatarajiwa kuleta mabadiliko chanya kwa wafanyakazi katika sekta binafsi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakihimiza maslahi bora. Ongezeko hilo linaongeza uwezo wa kununua mahitaji ya msingi kwa wafanyakazi, linachochea uzalishaji kutokana na kuimarika kwa motisha kazini, linaongeza uaminifu na uadilifu mahali pa kazi, na linasaidia kupunguza tofauti za kipato baina ya watumishi wa sekta ya umma na binafsi.

Amesisitiza kuwa waajiri katika sekta binafsi wanahimizwa kuhakikisha wanalizingatia kikamilifu tamko hili, kama sehemu ya wajibu wao wa kisheria na kijamii kwa wafanyakazi. Pia, Serikali itaendelea kushirikiana na waajiri pamoja na vyama vya wafanyakazi kuhakikisha kuwa haki za wafanyakazi zinalindwa, mazingira ya kazi yanaimarishwa, na maendeleo ya kiuchumi yanatokana na ushirikiano wa dhati.

"Wafanyakazi wetu ni nguzo kuu ya uchumi wetu. Hatuwezi kufikia Tanzania ya viwanda au uchumi wa kati ikiwa hatuwathamini. Kupitia hatua hii, tunathibitisha kwamba kazi siyo adhabu—ni heshima, na kila anayeifanya anastahili kulipwa kwa haki,” alisisitiza.
Wafanyakazi wa sekta binafsi, hasa wale walioko katika viwanda, migodi, kampuni za ulinzi binafsi, usafirishaji, huduma na kilimo cha kibiashara, wanatarajiwa kunufaika moja kwa moja na ongezeko hili.

Hatua hii ni ushahidi kwamba Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuwa sikivu kwa wananchi wake wote. Kwa mara nyingine, Tanzania inaweka historia ya kuwa nchi inayothamini kazi, wafanyakazi na maendeleo jumuishi.

Hatua hii ni ushahidi kwamba Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuwa sikivu kwa wananchi wake wote. Kwa mara nyingine, Tanzania inaweka historia ya kuwa nchi inayothamini kazi, wafanyakazi na maendeleo jumuishi.

📌Mwaka huu, kauli mbiu inayosimamia mchakato huu ni:

 ♻️“Sasa ni zamu ya sekta binafsi — Kazi ni Heshima, Mshahara Bora ni Haki.”

#UstawiWaMfanyakaziNiMsingiWaTaifaImara.
#TanzaniaMpyaHujengwaNaWafanyakaziWenyeMshaharaStahiki.
#SektaBinafsiBilaUnyonyaji,Inawezekana!  






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com