Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DK. SAMIA AENDELEA KUAHIDI UJENZI WA BARABARA ZA LAMI, KUONGEZA IDADI YA WATALII NA KUTATUA KERO YA WANYAMA WAKALI MANYARA


Na Jaliwason Jasson, BABATI 

MGOMBEA urais wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameahidi kujenga barabara kwa kiwango cha lami zilizoombwa na wagombea ubunge wa majimbo wa mkoa wa Manyara.

Dk. Samia alisema hayo leo Oktoba 4 wakati akiomba ridhaa ya kuchaguliwa tena ambapo alisema  wataendelea kujenga barabara za lami kwa kiwango cha lami ili kuunganisha mikoa.

Alizitaja barabara ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami kuwa ni Simanjiro mpaka Kongwa, Garbab mpaka Mbulu, Mogitu mpaka Haydom na barabara ya Nangwa/Gisamgalang mpaka Kongwa.
Dk. Samia alieleza kuwa wakipewa ridhaa  wataendelea kufungua barabara za vijijini ili kurahisisha usafirishaji wa mazao.

Katika hatua nyingine aliahidi kuongeza idadi ya watalii wa ndani na wa nje kutoka watalii milioni  5.3 miaka mitano iliyopita hadi kufikia watalii  zaidi ya milioni nane.

Vile vile aliahidi kuondoa tatizo la wanyama wakali linalosumbua wananchi wanaoishi vijiji vilivyopo jirani na Hifadhi za Taifa.

"Hatua tutakazochukua ni kujenga vituo vya kudhibiti wanyama wakali na tutachukua vijana wa vijijini wasaidiane na maafisa wa TAWA na TAWIRI,"alisema Dk. Samia.
 
Aliwaomba wananchi kuwa wavumilivu wakati serikali inajipanga kuchukua hatua.

Awali  wagombea ubunge  wa Kiteto Edward Ole Lekaita, James Ole Millya wa Simanjiro, Dk. Emmanuel Nuwas wa Mbulu vijijini, Zacharia Isaay wa Mbulu Mjini na Emmanuel Khambay wa Babati Mjini waliomba kujengewa barabara kwa kiwango cha lami huku mgombea wa ubunge wa Jimbo la Babati vijijini  Daniel Sillo akiomba vijiji 10 vilivyopo jirani na Hifadhi za Taifa ambavyo vinasumbuliwa na wanyama wakali akiomba kutatuliwa kwa changamoto hiyo.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com