Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA ULINZI NA USALAMA TANGA YAONYA DHIDI YA WANAOPANGA KUVUNJA AMANI SIKU YA UCHAGUZI



Na Mwandishi wetu,Tanga

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Tanga imetoa onyo kali kwa wananchi wote wenye nia ovu ya kuvunja amani katika kipindi cha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, ikisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayejihusisha na vitendo hivyo.

Onyo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Buriani, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga akiwa ameambatana na wajumbe wa Kamati ya Amani pamoja na viongozi wa vyama vya siasa mkoani humo.

Balozi Batilda amesema serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa mtu yeyote atakayehatarisha utulivu na amani ya mkoa huo, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu. Amesisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo, hivyo kila mwananchi anapaswa kuwa sehemu ya kulinda hali hiyo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, SACP Almachius Mchunguzi, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani na kuachana na vitendo vya uvunjifu wa sheria na taratibu za uchaguzi.

Kamanda Mchunguzi amesema jeshi la polisi limejipanga vizuri kuhakikisha usalama unakuwepo katika vituo vyote vya kupigia kura, na kwamba watakaothubutu kuvuruga amani watakumbana na mkono wa sheria bila huruma.

Kamati hiyo imewahakikishia wananchi wa Tanga kuwa maandalizi yote muhimu kwa ajili ya uchaguzi yamekamilika, huku ikitoa wito kwa wakazi wa mkoa huo kushiriki kikamilifu katika zoezi la uchaguzi kwa utulivu, nidhamu na uzalendo.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com