Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TEKNOLOJIA YAZIDI KUFUNGUA FURSA: ELIMU YA WATU WAZIMA YASISITIZWA KATIKA MAADHIMISHO YA WIKI YA ELIMU YA WATU WAZIMA WILAYA YA ARUSHA




Na Bora Mustafa - Arusha

Katika maadhimisho ya juma la elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi yaliyofanyika leo Wilaya ya Arusha, wadau wa elimu wameeleza mafanikio, changamoto na kutoa wito wa kuongeza juhudi katika kukuza elimu jumuishi, hasa katika zama za kidigitali.


Mgeni rasmi wa maadhimisho haya, Afisa Tarafa ya Temi, Bi. Chausiku Quamo, amewasifu  walimu wanaofundisha katika mfumo wa elimu ya watu wazima, akisema wanajitolea kwa moyo mkubwa kuwaendeleza wanafunzi katika mazingira yenye changamoto nyingi.  

Alieleza kuwa enzi za nyuma, mwanafunzi aliyepata ujauzito alipoteza kabisa haki ya kuendelea na masomo. Hata hivyo, kupitia jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hali hiyo imebadilika na sasa wanafunzi hao wanarudishwa shuleni kupitia mfumo rasmi na usio rasmi wa elimu.

Aidha Bi. Chausiku aliwakumbusha washiriki kauli ya Mwalimu Julius K. Nyerere kwamba elimu inalenga kuondoa ujinga, umaskini na uadui, na akasisitiza kuwa kila Mtanzania ana wajibu wa kujifunza ili kujikomboa kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu:  
“Kukuza Kisomo Katika Zama za Kidigitali kwa Maendeleo Endelevu ya Taifa Letu,”  
alisema kauli hiyo inaakisi umuhimu wa kutumia teknolojia kama nyenzo ya kuimarisha elimu ya watu wazima na kuwawezesha kujitegemea.

Alihitimisha kwa kuwataka wanafunzi, hasa watoto wa kike, kuachana na vishawishi vinavyoweza kuvuruga ndoto zao, na badala yake wajikite kwenye elimu na mafunzo yatakayowasaidia kujikwamua kimaisha.

Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Watu Wazima Mkoa wa Arusha, Bw. Emanuel Mahundo, alieleza kuwa hadi sasa wamefanikiwa kutoa mafunzo kwa wanafunzi 165, wakiwemo wanaume na wanawake waliopatiwa elimu ya ujasiriamali, usalama barabarani na afya ya akili.  

Aliongeza kuwa tayari vituo mbalimbali vimesajiliwa rasmi katika mkoa huo, vikitoa elimu ya watu wazima kwa ufanisi, ingawa bado kuna changamoto za kifedha na miundombinu.

Kauli zao zimeungwa mkono na baadhi ya wanufaika wa elimu hiyo. Oliva Evance Shayo, mkazi wa Dodoma na aliyepata mafunzo mwaka 2017, alisema kuwa ujuzi alioupata umemsaidia kujiajiri kama fundi cherehani. Alitoa wito kwa wanawake wengine kuchangamkia fursa hizo.

Kwa upande wa Zamzam Omary Madame, mhitimu wa kidato cha nne aliyeshindwa kuendelea na elimu ya sekondari, alisema amejiunga na chuo cha mukeja mwaka huu ili kupata ujuzi wa ushonaji na matarajio yake ni kuanzisha ofisi yake binafsi. Aliiomba serikali kuwasaidia wahitimu wa elimu ya watu wazima kwa kuwapatia mikopo au vifaa vya kuanzia miradi yao.

Kwa upande mwingine, Songo Muree, mwanafunzi mwenye miaka 30, alieleza mafanikio yake tangu alipoanza darasa mwaka 2022 bila kujua kusoma wala kuandika. Kufikia 2024, ameweza kusoma na kuandika kwa ufasaha na sasa anaweza kuwasiliana na watu mbalimbali kwa maandishi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com