Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAANDISHI WA HABARI WAJENGEWA UWEZO KUHUSU MABADILIKO YA TABIANCHI KUELEKEA COP30

Mkurugenzi Mtendaji wa TMF, Dastan Kamanzi
Meneja Uendeshaji wa CAN Tanzania, Boniventure Mchomvu

Na Kadama Malunde - Morogoro

Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya redio, magazeti na mitandao ya kijamii wamepata mafunzo maalum kuhusu mabadiliko ya tabianchi kuelekea Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) unaotarajiwa kufanyika Novemba 10–21, 2025 mjini Belem, Brazil.

Mafunzo hayo ya siku tatu (Oktoba 22–24, 2025) yaliyofanyika mkoani Morogoro yalilenga kuongeza uelewa wa waandishi wa habari kuhusu namna bora ya kuripoti masuala ya mabadiliko ya tabianchi kwa kuhusisha ajenda za kitaifa na kimataifa katika mjadala wa maendeleo endelevu.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Tanzania Media Foundation (TMF) kwa ushirikiano na Oxford Policy Management (OPM) kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Uingereza na Uswisi, huku Climate Action Network Tanzania (CAN) ikitoa utaalamu wa kitaalamu kuhusu masuala ya tabianchi na mchakato wa maandalizi ya mkutano huo wa kimataifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa TMF, Dastan Kamanzi, amesema mpango huo unalenga kuongeza ubora wa uandishi wa habari za tabianchi na kuhakikisha taarifa zinazochapishwa zinachochea mijadala ya kisera na uwajibikaji katika utekelezaji wa mikakati ya kitaifa kuhusu tabianchi.

“Tunataka kuona waandishi wanakuwa na uelewa wa kina kuhusu ajenda za COP30, ili waandike habari zenye ushawishi, zinazoelimisha na kuhamasisha hatua kwa jamii. Hii ni nafasi ya kuonyesha uwezo wa vyombo vya habari katika kuibua mijadala yenye manufaa kwa taifa,” ameongeza Kamanzi.

Kwa upande wake, Meneja uendeshaji kutoka shirika lisilo la kiserikali Climate Action Network Tanzania(CAN), Bonaventure Mchomvu, amesema COP30 ni fursa muhimu kwa Tanzania kuonyesha hatua ilizofikia na kueleza dunia namna inavyotekeleza mikakati yake ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Kupitia mkutano huu, Tanzania itapata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika mijadala ya kimataifa, kufuatilia ahadi zilizotolewa awali na kuwasilisha vipaumbele vipya vinavyolenga kuongeza uthabiti wa jamii na kupunguza uzalishaji wa hewa chafu,” amesema Mchomvu.

Ameeleza kuwa mafunzo kwa waandishi wa habari ni hatua muhimu ya kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi kuhusu mkutano huo na matokeo yake kwa Watanzania.

Mkutano wa COP (Conference of the Parties) ni jukwaa kuu la kimataifa chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) linalokutanisha nchi wanachama kujadili hatua za pamoja za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi duniani.

Mkutano wa mwisho, COP29, ulifanyika mwaka 2024 mjini Baku, Azerbaijan, ambapo washiriki walijadili masuala muhimu kuhusu fedha za tabianchi, utekelezaji wa ahadi za kupunguza hewa ukaa na ushirikiano wa kimataifa.

Mkutano wa mwaka huu, COP30, unatarajiwa kujikita katika kuimarisha utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa awali, huku Tanzania ikitarajiwa kuwasilisha mafanikio na vipaumbele vyake katika nyanja za nishati safi, usawa wa kijinsia na uhimilivu wa jamii dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com