
Na Bora Mustafa Fadhili - Arusha
Wananchi na viongozi mbalimbali wa Jiji la Arusha wamejitokeza kwa wingi kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Usafi Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini humo, kwa kufanya zoezi la usafi kuanzia eneo la Mianzini hadi Stendi Kuu ya mabasi.
Mama Yusuph, mfanyakazi wa Suma JKT, amesema zoezi limeenda vizuri na kwamba linasaidia kulinda mazingira kwa kuondoa taka ngumu na laini, hivyo kuweka mazingira katika hali nzuri kwa ajili ya afya ya watu wote. Hata hivyo, alieleza changamoto wanazokutana nazo kama vile magari yaliyopaki katika maeneo ya usafi, hali inayowalazimu kuwatafuta wamiliki ili kuyatoa.
Naye Sayona Bakar, mmoja wa washiriki, alisema wamefurahia kushirikiana na watu mbalimbali kwani zoezi limeenda vizuri na kwa wakati. Amepongeza mwitikio mkubwa wa wananchi na kusisitiza kuwa jitihada hizi ziendelee kwa maendeleo ya afya ya jamii.
Kwa upande wa uongozi, Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Deborah Manase, amesema kaulimbiu ya mwaka huu ni "Tunza Mazingira, Taka Ziwe na Thamani." Amewashukuru wananchi waliojitokeza na kusisitiza umuhimu wa kutunza mazingira kwa kukusanya taka zote kwani kwa wengine ni chanzo cha kipato.
Amesisitiza pia kuwa zoezi la usafi liendelee kila Jumamosi kama sehemu ya utamaduni wa kulinda afya za jamii.
Akihitimisha zoezi hilo, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo, amesema lengo la zoezi hilo ni kuthaminisha taka kwani si kila taka inapaswa kutupwa. Alitaja mfano wa chupa za plastiki, karatasi na maboksi kuwa vinaweza kurejeshwa kwenye ubora wake na kutumika tena kama mbadala.



Social Plugin