Septemba 10 ya kila mwaka huadhimishwa kote ulimwenguni kama Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Kujiua (World Suicide Prevention Day) siku inayowaenzi wale tuliowapoteza na kuleta matumaini kwa wale wanaopambana kimya kimya na matatizo yao.
Siku hii pia inatukumbusha kuwa kila maisha ni ya thamani na hivyo kuepuka kukata tamaa bali kuangalia namna nyingine ya kushughulikia changamoto za maisha.
Ni siku ya kutazama ndani zaidi ya macho ya watu, kuona huzuni iliyojificha nyuma ya tabasamu, na kuamua kuwa sauti kwa wale ambao wamechoka kunyamaza.
Takwimu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa zaidi ya watu 700,000 hujiua kila mwaka na mtu mmoja kila baada ya sekunde 40.
Kwa kila kisa kimoja cha kujiua, takriban watu 20 hujaribu kujiua(WHO, 2021), Takwimu hizi si tu namba ni ndugu zetu, marafiki zetu, wenzetu kazini, au pengine ni watu tuliokutana nao jana.
Ni watu waliopitia maumivu ya ndani ambayo hawakuweza kuyasema kwa sauti na pengine wanaona hawana hata wa kumwamini kuelezea hisia na maumivu waliyonayo.
Mara nyingi, hadithi ya huzuni huanza kwa kimya.
Wanaopambana na mawazo ya kujiua huwa hawapigi kelele badala yake, wanaendelea na maisha kama kawaida, huku wakibeba giza lisiloonekana.
Wengine hutuma ujumbe wa mwisho kwa namna zisizoeleweka na wengine kutotuma ujumbe kabisa, kujitenga ghafla, au kuandika maneno ya kuaga bila kusema moja kwa moja.
Ndiyo maana siku kama leo inatufundisha kuwa kila mtu tunayekutana naye anapigana vita tusiyoiona hivyo tusihukumu, tusibeze, tusipuuze wala kuwaumiza wengine.
Lakini kuna tumaini,Watu wengi waliowahi kufikiria kujiua lakini wakapona, hushuhudia kuwa mawazo yale yalikuwa ya muda.
Walihisi kuzama, lakini walipopata mtu wa kuwasikiliza, mshikamano, au hata muda tu wa kusubiri waliona nuru nyingine.
Kuzuia kujiua si jukumu la wataalamu wa afya ya akili pekee,ni kazi yetu sote,kila mmoja wetu anaweza kuwa taa ndogo inayoangazia giza la mwingine kwa kusikiliza bila kuhukumu, kwa kuwepo tu, au kwa kutoa ushauri.
Tunaweza kuwa sababu ya mtu kusubiri dakika tano zaidi ambazo zinaweza kuwa tiketi ya maisha mapya.
Leo tunawakumbuka waliopotea,tunawakumbatia waliobaki huku tunawainua waliopona lakini zaidi ya yote, tunatoa ujumbe wa moja kwa moja kwamba Usikate tamaa,Usife kimya,Wewe ni muhimu,Dunia bado haijamaliza kukupenda.
Nakukumbusha tu kuwa Watu hufikia hatua ya kujiua si kwa sababu wanataka kufa, bali kwa sababu wanataka maumivu waliyonayo yaishe.
Sababu kubwa zinazochangia ni pamoja na msongo wa mawazo, unyogovu (depression), matatizo ya kifamilia au kifedha, unyanyapaa wa afya ya akili, ukosefu wa msaada wa kijamii, na mara nyingine, matumizi ya dawa za kulevya au pombe.
Maumivu haya huwa ya ndani, yasiyoelezeka kwa urahisi, na mtu hujikuta akihisi kuwa hana njia nyingine zaidi ya kujiondoa kabisa.
Suluhisho pekee ni kutengeneza jamii inayoelewa na kuthamini afya ya akili na kuondoa unyanyapaa, kufundisha watu jinsi ya kutambua viashiria vya matatizo ya kisaikolojia, na kuhimiza mazungumzo ya wazi bila hukumu.
Aidha huduma za ushauri nasaha zipatikane kwa urahisi, lakini zaidi ya yote, kila mmoja wetu awe sehemu ya suluhisho kwa kusikiliza, kuwa karibu, na kuonyesha upendo usio na masharti.
Maisha yana changamoto, lakini hakuna changamoto isiyopungua nguvu mbele ya msaada wa kweli na mshikamano wa kibinadamu.
Imeandaliwa na Dotto Kwilasa.






Social Plugin