Pichani ni Erika Kirk na mumewe Charlie Kirk rafiki na shujaa wake ambaye amekuwa sababu ya kuufunza ulimwengu kuchagua msamaha badala ya chuki.
Imeandaliwa na Dotto Kwilasa, Septemba 21, 2025
Mke wa marehemu Charlie Kirk, Erika Kirk, ameibua hisia nzito katika mazishi ya mumewe baada ya kutangaza hadharani kuwa amemsamehe kijana anayetuhumiwa kumuua.
Akiwa mbele ya maelfu ya waombolezaji waliokusanyika kwenye State Farm Stadium, Glendale, Arizona, Erika amesema chuki haiwezi kujibiwa kwa chuki bali kwa upendo na msamaha.
“Leo ninachagua msamaha,” amesema kwa sauti ya kujikaza huku akibubujikwa na machozi,“Muuaji wa mume wangu hatapimwa kwa chuki yangu, bali ataachwa kwenye mikono ya Mungu.
Nafanya hivi kwa sababu Mume wangu Charlie alikuwa anaamini katika upendo na nguvu ya msamaha, nami naendelea na urithi huo.”amesisitiza
Mazishi hayo yamehudhuriwa na umati unaokadiriwa kufikia zaidi ya 90,000, na wengine maelfu walifuatilia nje ya uwanja na kupitia matangazo ya moja kwa moja.
Tukio hilo limewavutia viongozi wakuu wa kisiasa akiwemo Rais wa zamani Donald Trump, Makamu wa Rais JD Vance, pamoja na maseneta mashuhuri akiwemo Marco Rubio, ambao wote walitoa heshima zao kwa marehemu.
Charlie Kirk, mwanzilishi wa shirika la mrengo wa kulia Turning Point USA, aliuawa 10 Septemba 2025 katika chuo cha Utah Valley University wakati akihutubia wanafunzi.
Mshukiwa, Tyler James Robinson mwenye umri wa miaka 22, alifikishwa mahakamani akikabiliwa na mashitaka ya mauaji ya kukusudia, kutoa risasi kiholela na kujaribu kuzuia ushahidi tukio lililoibua mjadala mpana kuhusu usalama wa mikutano ya kisiasa na vyuo vikuu.
Baada ya kifo cha mumewe, Erika Kirk aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji (CEO) wa Turning Point USA, hatua iliyokuwa imeandaliwa mapema na marehemu.
Kuteuliwa kwake kunalenga kuhakikisha uendelevu wa shirika hilo lililoasisiwa na Charlie zaidi ya miaka kumi iliyopita.
Katika hotuba yake, Donald Trump amemtaja Charlie Kirk kama shujaa wa imani na uhuru, akisema mchango wake katika siasa za vijana Marekani hautasahaulika.
“Charlie alikuwa mtu wa watu,Kifo chake ni pigo kwa taifa letu,” amesema Trump.
Makamu wa Rais JD Vance naye alisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kitaifa, akieleza kuwa tukio la mauaji limeonesha kwa mara nyingine hatari ya siasa za chuki na mgawanyiko.
Tukio hilo limekuwa gumzo kubwa katika vyombo vya habari vya kimataifa, hasa kutokana na ujumbe wenye nguvu ya msamaha kutoka kwa Erika.
Wataalamu wa masuala ya kijamii na dini wameueleza msamaha huo kama “mfano wa kipekee wa imani na uthabiti wa kimaadili” katika nyakati ngumu.
Aidha, vyombo vya habari vimeibua mjadala kuhusu mustakabali wa siasa za Marekani, hususan nafasi ya Turning Point USA chini ya uongozi mpya wa Erika, pamoja na changamoto za kudhibiti matamshi ya chuki na usalama wa mikutano ya umma.
Charlie Kirk, aliyekuwa na umri wa miaka 31, aliwahi kuonekana kama sauti yenye ushawishi mkubwa miongoni mwa vijana wa kihafidhina nchini Marekani ambapo Kupitia Turning Point USA, alihimiza ushiriki wa vijana katika siasa, akilenga kulinda misingi ya uhuru wa kiuchumi na imani ya kidini.
Mazishi yake (memorial/funeral service) yalifanyika Jumapili, tarehe 21 Septemba 2025, kwenye State Farm Stadium, Glendale – Arizona, Marekani, yakihudhuriwa na maelfu ya watu pamoja na viongozi wa kitaifa na kuacha alama kubwa si tu kwa familia na wafuasi wake, bali pia kwa mjadala mpana wa hali ya siasa na mshikamano wa jamii katika taifa hilo na duniani kwa u jumla.




Social Plugin