Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ISSA KURUDISHA HESHIMA YA JIJI LA TANGA KUPITIA ACT WAZALENDO, TAYARI KACHUKUA FOMU INEC

Na Hadija Bagasha Tanga, 

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Tanga mjini kwa tiketi ya ACT Wazalendo Seif Issa Abdallahassan amesema anawania nafasi hilo ili kurudisha heshima ya jiji la Tanga katika kufanya maamuzi sahihi ambayo ilipotea kwa muda mrefu.

Ameyasema hayo leo katika Halmashauri ya jiji hilo aliporudisha fomu ya uteuzi kwamba kikubwa ni kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo sambamba na kuwapatia vijana ajira kwa kurudisha viwanda vilivyokufa pamoja na kuimarisha uchumi.

"Huu ni mji uliokuwa uliongoza kwa viwanda na ndio ulioongoza kwa ajira na uchumi kabla na baada ya uhuru, lakini sasa vijana wetu hawana ajira za kutosha, Tanga ni moja ya Majiji matano nchini ukiacha Dar es salaam ambako kuna bahari kama hapa,

"Majiji mengine yote uchumi umeendelea na Tanga limekuwa jiji la mwisho kiuchumi, na hili siyo jambo linalotokana na mazingira bali kuna viongozi ambao siyo wabunifu na hawaumizwi na maisha ya wananchi" ,amesema Issa.

Sambamba na hayo pia amebainisha kwamba suala la miundombinu bado kuna baadhi ya maeneo ni kero hasa kipindi cha mvua, lakini pia amedhamiria kuwasimamia wanawake katika suala Zima la upatikanaji wa mikopo ya halmashauri kwakuwa bado usimamizi wa upatikanaji wake ni mgumu kwao.

Mteule huyo wa Chama Cha ACT-Wazalendo amesema ameamua kujitosa katika nafasi hiyo Ili aweze kutumia uwezo wake kusukuma maendeleo ya Tanga ambayo yamekuwa yakididimia kila siku.

Amesema amesoma nyaraka za mipango ya maendeleo ya kuanzia mwaka 2020-2025 ya Halmashauri ya Jiji la Tanga na kubaini kuwa ni mizuri lakini haijatekelezwa kwa kukosa usimamizi na ufuatiliaji wa fedha za maendeleo zinazotolewa na Serikali.

"Miaka ya kupatikana Uhuru,Tanga ilikuwa na kila kitu,viwanda,kilimo cha mkonge,bandari yenye ufanisi soka na michezo mbalimbali lakini sasa hivi ni Jiji la mwisho kati ya majiji yaliyopo Tanzania kwa maendeleo sababu kuu ni kukosa usimamizi na ufuatiliaji wa fedha za maendeleo"amesema Abdallahasan.

Kwa upande wa wanawake, mgombea huyo amesema wamekuwa wakinyonywa na mikopo umiza inayotokana na sera mbovu zisizowajali wajasiliamali wa hali ya chini.

"Leo siyo siku ya kusema kwa sababu nimerejesha fomu naisubiri kupitishwa... tutazungumza mengi kwenye  kampeni,nimeamua kuwania ubunge li niweze kusukuma maendeleo",amesema Abdallahasan 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com