
Zaidi ya hati miliki za kimila 1,200 zimetolewa kwa wananchi wa vijiji vya Idukilo na Mwadui Lohumbo katika Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga.
Zoezi hilo limefanyika kupitia mpango wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi, ambao unalenga kutatua changamoto ya migogoro ya ardhi vijijini na kuwawezesha wananchi kumiliki ardhi yao kisheria.
Zoezi hilo limefanyika leo Julai 09,2025 katika vijiji vya Idukilo na Mwadui Luhumbo halmashauri ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Akizungumza katika tukio hilo, Afisa Mifumo kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi, Jofrey Kakuru, amesema kuwa lengo kuu la tume hiyo ni kuhakikisha kila mwananchi anamilikishwa ardhi yake kwa mujibu wa sheria, ili kumuwezesha kuendesha maisha ya kiuchumi kwa utulivu na bila migogoro.
“Tunataka kuona wananchi wanakuwa na usalama wa miliki, wanapanga matumizi bora ya ardhi na hatimaye wanainuka kiuchumi kwa kutumia ardhi hiyo kama mtaji,” amesema Kakuru.
Kwa upande wake, Msimamizi wa zoezi la uandaaji wa hati za kimila, Eduward Mpanda, amewahamasisha wananchi wa vijiji vya Idukilo na Mwadui Lohumbo kujitokeza kwa wingi wakiwa na nyaraka zao muhimu ili wapate hati miliki hizo bila kutozwa gharama yoyote.
“Zoezi hili ni bure kabisa. Tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi ili wanufaike na mpango huu wa serikali wa kuwapatia hati miliki za kimila ambazo zitawasaidia hata kupata mikopo kwa ajili ya kujiinua kiuchumi,” amesisitiza Mpanda.
Naye Mratibu wa Timu ya Matumizi Bora ya Ardhi ambaye pia ni Afisa Ardhi Mteule wa Wilaya ya Kishapu, Grace Pius, ameeleza kuwa mpango huu umefanikiwa kutatua migogoro ya muda mrefu hasa kwa wananchi waliokuwa wakiishi karibu na maeneo ya mgodi, waliokuwa kwenye mgogoro wa mipaka na matumizi ya ardhi.
“Kupitia mipango hii ya matumizi bora ya ardhi, wananchi sasa wanaelewa ni maeneo gani ya makazi, kilimo, malisho au biashara na hivyo migogoro imepungua kwa kiwango kikubwa,” amesema Grace.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuimarisha usimamizi wa rasilimali ardhi, kuondoa migogoro ya umiliki, na kuhakikisha maendeleo endelevu yanapatikana kwa wananchi hasa wa maeneo ya vijijini.





Social Plugin