Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SAMIA DAY:SHULE, MAJI VYABADILI MAISHA YA WANAFUNZI KONDOA



Na Dotto Kwilasa, Kondoa

Wilaya ya Kondoa imeungana na maeneo mengine ya Mkoa wa Dodoma kuadhimisha siku maalum ya kutambua mchango wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan (Samia Day), katika kusukuma mbele ajenda ya maendeleo jumuishi kwa vitendo.

Tofauti na maadhimisho mengine, Kondoa imeadhimisha siku hiyo kwa kufanya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya kijamii, ikiwemo afya, elimu, maji na barabara, kama njia ya kupima utekelezaji wa sera na mipango ya serikali katika ngazi ya chini.

Maadhimisho hayo yamebeba uzito wa kisera na kiutendaji, yakilenga kuonesha namna dhamira ya Rais Samia inavyotekelezwa katika maeneo ya pembezoni, mbali na majukwaa ya mijini.

Katika maadhimisho hayo, viongozi wa mkoa na wilaya wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Fatma Almasi Nyangasa, wametembelea miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo sekta ya elimu, afya, maji na barabara.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Kaimu Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Dodoma, Julieth Isdor, ameeleza kuwa hadi sasa mkoa umetekeleza miradi 253 yenye thamani ya shilingi bilioni 42.5, ambapo zaidi ya bilioni moja zimetokana na mapato ya ndani.

Amesema mafanikio hayo yote yametokana na juhudi za Serikali ya awamu ya Sita chini ya Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuwajali na kuwatumikia wananchi.

Isdor ametumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi kuitunza na kuithamini miradi yote,“Wananchi wanapaswa kuilinda miradi hii ili idumu kwa muda mrefu, kwani maendeleo ni mchakato unaohitaji utulivu,nawaomba wananchi waendelee kuwa na imani kwa Serikali,” amesema

Akizungumzia utekelezaji wa Nishati safi kama ajenda ya kitaifa, amebainisha kuwa Serikali imesambaza zaidi ya mitungi 200 ya gesi kwa wananchi Wilayani Kondoa, hatua inawasaidia wanawake kupika kwa wakati na kuondokana na athari za moshi wa kuni.

Naye Afisa Elimu wa Kata ya Mnenia, Stanley Mtavangu, amezungumzia Ujenzi wa Shule ya Sekondari Mnenia na kueleza kuwa Shule hii mpya ambayo ni zawadi ya Rais Samia kwa wanafunzi imejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 544.2, ikijumuisha jengo la utawala, vyumba vya madarasa, maabara, maktaba, chumba cha TEHAMA, tanki la maji, na vyoo.

Amesema awali, mradi huo ulianzishwa kwa nguvu za wananchi kwa thamani ya shilingi milioni 20, ukapata ufadhili kutoka TASAF wa shilingi milioni 113 na kueleza kuwa hayo ni mafanikio makubwa kwa kuwa wananfunzi wamepata afueni.

“Awali wanafunzi walitembea zaidi ya kilomita 14 kwenda shule,wengi walikuwa wakichelewa madarasani, walichoka, na wengine walikumbwa na vishawishi njiani kama bodaboda na utoro. Sasa tuna wanafunzi 114 wanaosoma karibu na nyumbani,” amesema Mtavangu.


Mradi mwingine ni Kituo cha Kukusanyia Maziwa – Mafai, Kata ya Haubi
Mradi huu uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.5 unalenga kuongeza thamani ya mazao ya mifugo kwa kuimarisha ukusanyaji na uhifadhi wa maziwa.

Msimamizi wa Mradi huu Ramia Ally Omary amesema Licha ya uzalishaji kuwa mkubwa, maziwa mengi yanakosa mnunuzi, hivyo kuhitaji ushiriki wa wawekezaji binafsi kwenye Kituo hicho.

"Tunamshukuru sana Rais wetu Mama Samia kwa kutupatia mradi huu, lakini changamoto kubwa imebaki kuwa ukosefu wa soko la uhakika kwa bidhaa hii ya maziwa,uzalishaji ni makubwa lakini soko hakuna tunaomba Serikali ituwezeshe kufanikisha hili, " ameeleza Msimamizi huyo wa mradi.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Masange, Rajab Isaka, amesema kuwa juhudi za serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo zimeleta matumaini makubwa kwa wananchi waliokuwa wakikosa huduma muhimu kwa muda mrefu, hususani katika sekta za elimu, afya na miundombinu ya maji.

Amesema Samia Day ni siku muhimu kuenzi miradi yote ya maendeleo na kufafanua kuwa kabla ya miradi hiyo kutekelezwa, wananchi walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo, hali iliyosababisha usumbufu mkubwa na kuchelewesha shughuli za maendeleo ya familia.

“Leo hii tunashuhudia watoto wetu wakisoma karibu na makazi yao, akinamama wakijifungua katika mazingira salama, na kila kaya ikipata maji safi kwa urahisi haya yote ni matokeo ya jitihada za dhati za Serikali ya Awamu ya Sita,” ameeleza Isaka.

Licha ya ni miradi hiyo yenye sura ya mafanikio ya Serikali ya awamu ya Sita, kuna miradi mingine mingi ya kimakakati Wilayani Kondoa ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Mnenia,mradi unatekelezwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 2.4 na umefikia asilimia 85 ya utekelezaji.

Mradi huu Unajumuisha jengo la OPD, maabara, wodi za kulaza wagonjwa, chumba cha upasuaji na jengo la mama na mtoto na unatarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 100,000 kutoka kata nane za wilaya hiyo.

Mradi mwingine ni wa Maji – Kinyasi
ambao umeleta mabadiliko makubwa kwa wakazi wa vijiji vya Kinyasi, Mwaikisabe na Bukulu ambapo Kupitia tanki la maji lenye ujazo wa lita 150,000 na mtandao wa mabomba wa zaidi ya kilomita 6, wananchi zaidi ya 7,000 sasa wanapata huduma ya maji safi na salama.

Miradi mingine ni Kituo cha Afya – Pahi ambapo ujenzi wake umekamilisha majengo ya OPD, chumba cha kujifungulia na nyumba ya mtumishi mmoja na tayari wananchi wameanza kupata huduma muhimu za afya, huku mpango ukiwekwa kuongeza idadi ya wahudumu na vifaa tiba ili kuboresha zaidi utoaji wa huduma.

Kwa upande wa Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mnemia wamesema ujenzi wa shule hiyo karibu na makazi yao umewasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uchovu na kuongeza muda wa kujisomea.

Fauza Kisinini mwanafunzi wa kidato cha pili, amesema kuwa hapo awali alilazimika kuamka saa kumi alfajiri na kutembea kilomita zaidi ya kumi kufika shuleni na kupelekea kuichukia shule.

“Nilikuwa naamka mapema sana na nikifika darasani ninakuwa nimechoka nasinzia ,Sasa najifunza vizuri, nawahi shule na hata muda wa kurejea nyumbani ni mzuri,tunapata muda mwingi wa kufurahia na familia zetu,namshukuru sana Mama Samia kwa shule hii,” amesema

Naye Salum Daudi, mwanafunzi wa kidato cha kwanza, amesema kuwa uwepo wa shule hiyo umewaepusha na hatari za barabarani na kuwapa amani ya moyo hata wazazi wao.

“Tulikuwa tukikatiza maporini, kuna nyakati tuliwahi kuvamiwa na mbwa porini,lakini sasa tuko salama Wazazi wetu hawana hofu tena kwa sababu tuko karibu, tunasoma kwa amani,” amesema Salum deni limebaki kwetu nalo ni kusoma kwa bidii kutimiza ndoto zetu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com