Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Kukosekana kwa maelewano kati ya baba na mama ndani ya familia kunatajwa kuwa chanzo kikubwa cha watoto wengi vijijini kukosa haki zao za msingi, ikiwemo malezi bora na fursa ya kupata elimu, hali inayowasukuma kujiingiza kwenye makundi hatarishi na kuacha masomo.
Hayo yamebainika mwishoni mwa wiki katika mdahalo wa kijamii uliofanyika katika Kijiji cha Kidoka, wilayani Chemba, mkoani Dodoma, ambapo viongozi wa kimila, viongozi wa dini, akina mama, vijana, pamoja na wawakilishi wa serikali za vijiji na mashirika ya kiraia walijadili kwa kina changamoto zinazokwamisha usawa wa kijinsia na ustawi wa familia.
Mdahalo huo uliandaliwa kupitia mradi wa Tuinuke kwa Pamoja kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland, ambapo washiriki walisema kuwa familia nyingi zimepoteza mwelekeo kutokana na migogoro ya wazazi, hali ambayo huathiri maendeleo ya watoto, hususan elimu na malezi bora.
“Tumeona watoto wengi wa kiume na wa kike wakijihusisha na biashara za pombe, kuuza miili yao, na wengine kukimbilia mijini kusaka ajira zisizo rasmi,wote hawa ni waathirika wa migogoro ya nyumbani,” amesema Mzee Ahumani Twalib, mmoja wa wazee wa kijiji.
Naye Hamida Ndwatta ameeleza kuwa uwepo wa vilabu vya pombe kwenye makazi ya watu kumechangia wazazi Wengi kuishia kuwa walevi na kushindwa kutimiza majukumu yao ya malezi.
Amesema kuwa baadhi ya mila na desturi kama unyago na jando zimegeuka kuwa chanzo cha mimba za utotoni, utoro wa shule, na ndoa za utotoni, mambo yanayovunja kabisa ndoto za vijana wengi wa vijijini.
" familia ni msingi wa maendeleo ya mtoto, hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa wazazi wanapata elimu ya malezi na kushirikiana kwa usawa ili kujenga kizazi chenye maadili na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa, "ameeleza
Kwa ujumla ameeleza kuwa ustawi wa familia si suala la huduma pekee, bali linahitaji jitihada za kijamii, kimila, kielimu na kiuchumi ili kumjenga mtoto wa Tanzania anayejitegemea na kuchangia katika maendeleo endelevu.
Kwa upande wake, Vera Assenga kutoka TGNP, amesisitiza kuwa si kila mila ni potofu, bali ni muhimu kuchuja yale mafundisho yanayokinzana na haki na ustawi wa watoto.
"Ngoma za utamaduni zinaweza kubaki kama sanaa, lakini maudhui yake yafanyiwe marekebisho. Tukiweka sheria rafiki kwa mtoto wa kike, tutaweza kulinda maisha yao na bado tukadumisha utamaduni wetu,” amesema.
Deogratius Temba, mwezeshaji wa mradi wa Tuinuke kwa Pamoja, amesema mijadala kama hiyo inalenga kuamsha jamii kijamii na kiakili ili kuchukua hatua za kubadili mwenendo wa mila na desturi zinazodhuru watoto.
Mdahalo huo umeibua mwamko mpya katika wilaya ya Chemba mwamko wa kuhoji, kuchuja, na kubadili mila zenye madhara kwa watoto. Ni wazi sasa kuwa jamii hiyo inahitaji mabadiliko ya haraka, ili kuwapa watoto nafasi ya kutimiza ndoto zao bila vikwazo vya kimila.
Social Plugin