
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Mhe. Masele ambaye aliwahi kulitumikia jimbo hilo kwa mafanikio kwa kipindi cha miaka 10 (2010–2020), amesema ameamua kujitosa tena katika kinyang’anyiro hicho ili kurejesha matumaini, mshikamano, na maendeleo kwa wananchi wa Shinyanga Mjini.
“Nataka nirudishe furaha iliyotoweka. Wananchi wa Shinyanga wana haki ya kumchagua kiongozi wanayemtaka, si kulazimishiwa mtu wasiyempenda. Hiyo ni sawa na kumlazimisha mtu kula makande wakati anataka biriani ya kuku,” alisema Masele kwa msisitizo.
Aahidi Maendeleo ya Kimkakati
Mhe. Masele ameweka bayana vipaumbele vyake endapo atapata ridhaa ya kuwa Mbunge, akitaja ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo:
* Kukamilisha haraka mradi wa Soko Kuu la Shinyanga ambao umekwama kwa muda mrefu;
* Kupanua na kuboresha miundombinu ya barabara muhimu ikiwemo ya kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwawaza;
* Kuirejesha Stand United Ligi Kuu kwa lengo la kuinua michezo na vipaji vya vijana jimboni;
* Kuhakikisha miradi iliyokwama inafufuliwa kwa weledi na kwa maslahi ya wananchi.
“Shinyanga haihitaji mwanaharakati, inahitaji kiongozi mwenye uzoefu wa kweli wa kisiasa na kiuongozi. Haya si mambo ya majaribio.”
Rekodi ya Uongozi na Maadili
Masele amesema amelelewa katika misingi imara ya uongozi ndani ya CCM, na amehudumu kwenye nafasi mbalimbali za juu za kitaifa na kimataifa:
Spika wa Bunge la Afrika (Pan African Parliament),
Naibu Waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.
Amesisitiza kuwa uongozi unahitaji mafunzo, nidhamu na malezi ya kisiasa, na kwamba anayo rekodi safi ya utendaji yenye kuacha alama popote alipohudumu.
“Shinyanga haihitaji kiongozi muongo, mchonganishi, wala tapeli wa kisiasa. Wananchi hawataki kufokewa kama watoto. Wamechoka na viongozi wa kuletewa. Wanataka chaguo lao.”
Historia ya Kura za Maoni
Mwaka 2020, Masele ndiye aliyeongoza katika kura za maoni za CCM kwa ushindi wa kishindo, huku mbunge wa sasa akishika nafasi ya saba kwa kupata kura 12 pekee.
Mhe. Masele amesema ana imani kubwa kuwa wananchi na wanachama wa CCM Shinyanga Mjini bado wana kiu ya kumuona kijana wao akirejea kuongoza tena kwa kasi, maarifa, na mshikamano wa kweli.
“Kwa uzoefu wangu wa ndani na nje ya nchi, nitaleta maendeleo ya kweli kwa kushirikiana na viongozi wenzangu wa chama na serikali. Huu ni wakati wa kuandika upya historia ya Shinyanga.”
Social Plugin