Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TCRA KUENDELEA KUDHIBITI NAMBA TAMBULISHI KWA KUTUMIA KANZIDATA



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) imesema inaendelea kudhibiti namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano kwa kutumia Kanzidata, ambapo zaidi ya namba tambulishi 44,000 zilizohusishwa na wizi au udukuzi zilifungiwa.

Aisha udhibiti wa laini Haramu
Zaidi ya laini za simu 47,000 zilizuia kutokana na matumizi yasiyo halali, huku zaidi ya nambari 39,000 za NIDA zikiwekwa kwenye orodha ya kuzuiwa (blacklist), kwa kushirikiana na vyombo vya usalama.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt,Jabiri Bakari,amezungumza hayo Bungeni Dodoma Mei 16,2015 mara baada ya Bunge kupitisha bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari .

Amesema Ongezeko la Miamala ya Kidigitali katika kipindi cha Julai 2024 hadi Aprili 2025, iliongezeka kwa asilimia 24.7 na thamani ya miamala ilikua kwa asilimia 56.5, ikionyesha mafanikio ya usimamizi na matumizi ya TEHAMA katika malipo.

Licha ya hayo amesema kuwa Tanzania inazidi kupiga hatua katika maendeleo ya kidijitali, kufuatia ongezeko la haraka la laini za simu na watumiaji wa intaneti kote nchini.

"Kama waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa alivyosema hadi kufikia Aprili 2025, laini za simu zilizosajiliwa zimeongezeka hadi milioni 90.4 kutoka milioni 73.5 kwa kipindi kama hicho mwaka 2024, ikiwa ni ongezeko la asilimia 22.9," amesema.

Ameongeza kuwa watumiaji wa intaneti wameongezeka kwa asilimia 32.3, kutoka milioni 37.3 hadi milioni 49.3. Hii inaonesha namna Watanzania wanavyokumbatia teknolojia na kuitumia katika maisha yao ya kila siku.

"Mafanikio haya yametokana na kuongezeka kwa uwekezaji kwenye miundombinu ya mawasiliano, hasa minara ya simu ambayo imeongezeka kwa kasi kubwa katika maeneo ya mijini na vijijini," amesema na kuongeza;

"Tupo katika zama za uchumi wa kidijitali uchumi unaotegemea teknolojia ya mawasiliano na matumizi ya mitandao katika kila nyanja ya maisha yetu ya kila siku lakini pamoja na mafanikio hayo, kumekuwa na ongezeko la uhalifu wa kimtandao, jambo linalohitaji hatua za haraka," ameeleza.

Mkurugenzi huyo a mesema mamlaka hiyo imeendelea kutoa elimu kwa wananchi na kushirikiana na vyombo vya usalama ili kuhakikisha mitandao inabaki salama.

Pamoja na mambo mengine Kamati ya Bunge ya Miundombinu imetaka serikali kushughulikia kwa kina tatizo la utapeli wa kimtandao na jumbe zisizoombwa, kwa kushirikiana na makampuni ya simu na vyombo vya dola.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com