Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Ismail Ally Ussi akiweka jiwe la msingi katika shule ya msingi Chikukwe wilayani Masasi Mkoa wa Mtwara
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Ismail Ally Ussi akizungumza baada ya kufika katika Shule ya Msingi Chikukwe iliyopo Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara kabla ya kuweka jiwe la msingi katika shule hiyo
Shule iliyowekwa jiwe la msingi Chikukwe na Mwenge wa Uhuru Wilayani Masasi
Na Regina Ndumbaro Masasi-Mtwara
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Chikukwe iliyopo katika Wilaya ya Masasi wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia madarasa mawili mapya.
Shukrani hizo zimetolewa mara baada ya Mwenge wa Uhuru kuweka jiwe la msingi katika madarasa hayo mapya, hafla iliyoongozwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025, Ndg. Ismail Ally Ussi.
Katika hafla hiyo, Ndg. Ussi ameitaka jamii kushiriki kikamilifu katika kutunza miundombinu ya shule hiyo kwa ajili ya manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya wananchi na serikali ni msingi imara wa maendeleo ya sekta ya elimu nchini.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetumia kiasi cha shilingi 66,330,000 kukamilisha ujenzi wa madarasa mawili ya wanafunzi wa awali pamoja na ujenzi wa matundu sita ya vyoo katika shule hiyo.
Ujenzi huo unalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wa shule ya awali.
Mwenge wa Uhuru umekamilisha mbio zake katika halmashauri mbili za Wilaya ya Masasi ambazo ni Masasi TC na Masasi DC, ambapo miradi mbalimbali imetembelewa, kukaguliwa na kuonwa.
Ifikapo tarehe 20 Mei 2026, Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuelekea Halmashauri ya Wilaya ya Newala kuendelea na mbio zake.
Social Plugin