Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Fainali ya mashindano ya Polisi Jamii Cup yaliyoshirikisha timu 14 kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma yamehitimishwa kwa ushindani mkubwa kati ya timu za Mpunguzi na Chang’ombe, yakilenga kuhamasisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, hasa vijana.
Mashindano hayo yaliandaliwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi George Katabazi, kwa lengo la kujenga mahusiano bora kati ya jamii na Jeshi la Polisi, kuhamasisha utoaji wa taarifa za uhalifu, na kuzuia vijana kujiingiza katika vitendo viovu.
Akizungumza wakati wa fainali hizo zilizofanyika Mei 19, 2025, Katabazi alisema:
“Polisi Jamii Cup ni jukwaa muhimu kwa vijana kushiriki shughuli chanya. Tunawapa nafasi sio tu kuonyesha vipaji vyao bali pia kuwa sehemu ya mabadiliko katika jamii.”ameeleza
Katika kuhitimisha mashindano hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliwataka vijana kutumia fursa ya kujiandikisha katika daftari la wapiga kura pamoja na kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
“Tusiipoteze fursa hii muhimu. Vijana mjitokeze kwa wingi kujiandikisha na kugombea uongozi. Huu ndio wakati wa kufanya maamuzi ya maendeleo yenu na ya taifa,” amesema RC Senyamule.
Akimpongeza Kamanda Katabazi kwa juhudi za kuandaa mashindano hayo, Senyamule amesema kuwa michezo ni njia madhubuti ya kuhamasisha amani, mshikamano, na kushirikiana kwa ajili ya maendeleo ya jamii.
Ameeleza kuwa kila mechi ilikuwa na ujumbe wa kijamii, akiongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwa mfano kwa kuwekeza kwa vijana na kufurahia mafanikio ya michezo, kama vile timu ya Simba kufika fainali.
“Kupitia mashindano haya, kuna vijana wanaonekana na kupata fursa ya kiuchumi kupitia vikundi vitakavyosaidiwa na halmashauri. Michezo inafundisha nidhamu, mshikamano na thamani ya amani,” aliongeza Senyamule.
Aidha, amehimiza vijana kuacha maneno yanayoweza kuvuruga amani na badala yake kujikita katika kuchukua hatua za maendeleo.
Mashindano haya yameonekana kama sehemu ya maandalizi ya vijana kuelekea uchaguzi huku yakiimarisha mahusiano chanya kati ya Jeshi la Polisi na jamii.
Social Plugin