Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAKULIMA WAPONGEZA REDESO NA CARE INTERNATIONAL KUFANIKISHA NDOTO ZA WANANCHI WA KISHAPU KUPITIA UFUGAJI KUKU CHOTARA KITAALAMU

Picha ya pamoja ya watumishi kutoka Redeso,Care International,maafisa ugani ofisi ya Mkurugenzi,maafisa ugani wa wa vijiji vya mradi na wakulima na waelimishaji ngazi ya jamii walipomaliza kikao cha kuelimisha kuhusu ufugaji kuku chotara kisasa kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Veta Kishapu Mkoani Shinyanga Mei 29,2025
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kakola Kata ya Uchunga Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Lata Pungu akizungumza jinsi alivyonufaika na mafunzo kutoka Redeso na Care International ya ufugaji kuku chotara kisasa Mei 29,2025 Katika ukumbi wa Veta Kishapu

Na Sumai Salum – Kishapu

Baadhi ya wawezeshaji wa ngazi ya jamii na wanakikundi wa mradi wa ufugaji wa kuku chotara kwa njia ya kisasa kutoka Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga wamelipongeza shirika la Relief to Development Society (REDESO) kwa kushirikiana na CARE INTERNATIONAL kwa kuwapatia elimu ya kujiinua kiuchumi kupitia ufugaji kuku chotara kisasa na kilimo cha bustani.

Akizungumza katika kikao kilichofanyika leo Mei 29, 2025 katika ukumbi wa VETA wilayani humo Mwezeshaji ngazi ya jamii kutoka Kijiji cha Negezi Fredina Said amesema elimu waliyoipata imebadili fikra zao kuhusu njia za kujiletea maendeleo kupitia shughuli za kilimo na ufugaji kuku chotara kisasa.

“Huu ni mwanzo wa mapinduzi mapya mafunzo ya nadharia na vitendo yaliyotolewa yameleta mabadiliko makubwa ya fikra na mitazamo yetu juu ya shughuli za ufugaji tumejifunza kwa kina kuhusu ufugaji bora wa kuku wa kisasa, uchanganyaji wa chakula, njia bora za ulishaji na unyweshaji maji, na umuhimu wa kuwashirikisha wataalamu wa mifugo pindi kuku wanapopata changamoto za kiafya,” amesema Fredina kwa shukrani.

Kwa upande wake, Lata Pungu, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kakola na mnufaika wa mradi, amesema kuwa kupitia elimu hiyo ameweza kuelewa vizuri ujenzi wa banda bora, usafi wa mazingira ya banda na kuku, pamoja na kushirikiana na wafugaji wengine kwa lengo la kuongeza kipato kupitia uzalishaji wa kuku chotara kwa njia ya kisasa.

Afisa Mifugo na msimamizi wa mradi huo wilayani Kishapu, Bw. Damla A. Damla, amesema ujio wa mradi huo umeleta heshima kubwa kwa Wilaya na kuahidi kuwa ofisi yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na wafugaji kuhakikisha mafanikio zaidi.

Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya Kalekwa Mtoni ambaye pia ni mwezeshaji wa mafunzo hayo, amesisitiza kuwa mradi huo unalenga kuunga mkono azma ya Mkurugenzi wa Halmashauri Bw. Emmanuel Johnson ya kuwawezesha wananchi kupiga hatua ya maendeleo huku wakiboresha lishe ya familia zao.

“Hii elimu ni gharama wangeweza kuipeleka kwingine lakini wametuona sisi kuwa na thamani ni wajibu wetu kuhakikisha tunaitumia ipasavyo kuleta mabadiliko kuanzia ngazi ya familia hadi kijiji,” ameongeza Mtoni.

Meneja Mradi kutoka CARE International, Bw. Wilfred Makombe amewahimiza wanakikundi na wawezeshaji ngazi ya jamii kutojizuia kuanza miradi kwa kisingizio cha kukosa mabanda ya kisasa, bali watumie vifaa vinavyopatikana katika mazingira yao.

“Tumeshuhudia mafanikio kule Negezi na Busongo ambapo baadhi ya wanakikundi wameanza kwa kutumia vifaa vya kawaida kama bikobiko na wameshanufaika hivyo ni lazima kuweka malengo ya muda mfupi na kuyaanza mara moja”  amesema Makombe.

Mradi huu unaotekelezwa na REDESO Kishapu kwa ushirikiano na CARE International unatekelezwa katika vijiji 10 vya Wilaya ya Kishapu ambavyo ni: Shagihilu, Mihama, Busongo, Negezi, Uchunga, Kakola, Lubaga, Bubinza, Isoso na Unyanyembe.
Afisa ugani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Kalekwa Mtoni akiwasilisha mada ya namna ya kupeleka elimu Vijijini na Utarataibi wa utendaji kazi kwenye kikao cha elimu ya kijinga kiuchumi kupitia ufugaji kuku chotara kisasa kilichoandaliwa na Redeso wakishirikiana na Care International kwa wadau wa mradi huo Mei 29,2015 katika ukumbi wa Veta Kishapu.
Mwezeshaji ngazi ya jamii kutoka Kijiji cha Negezi Kata ya Ukenyenge Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Fredina Said akiwapongeza Redeso na Care International kwa elimu waliyowapa ya ufugaji kuku chotara kisasa Mei 29,2025 Katika ukumbi wa Veta Kishapu
Darasa likiendelea
Wakati wakiwasilisha mpango kazi wa utekelezaji ufugaji kuku chotara kisasa kuanzia mwezi Mei mwaka 2025 katika Vijiji vyote ya mradi
Meneja miradi Redeso Kishapu Charles Buregeya(kushoto),afisa wa Redeso Kishapu Erica Karuta(katikati) na Mratibu mradi kutoka Care International Wilfred Makombe(kulia) kwenye kilele cha mafunzo ya ufugaji kuku chotara kisasa yaliyofanyika ukumbi wa Veta Kishapu yakihusianisha waelimishaji ngazi ya jamii,wanakikundi,maafisa ubani ngazi ya Vijiji na Halmashauri ya Kishapu Mei 29,2025
Picha ya pamoja ya watumishi kutoka shirika la Redeso na Care International na maafisa ugani wa Kata na vijiji vya mradi wa kukabiliana na mabadiliko tabianchi katika ufugaji wa kuku chotara kisasa Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com