
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa ujumbe mzito kwa wajumbe wa chama hicho, akisisitiza umuhimu wa mchujo wa wagombea kufanyika kwa haki, uadilifu na kwa kuzingatia maslahi ya chama na taifa kwa ujumla.
Katika hotuba yake ya kufunga Mkutano Maalum wa CCM uliofanyika Mei 30, 2025 – kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Dkt. Samia ameeleza kuwa si kila mtu anayejitokeza kuwania nafasi za uongozi anastahili kupitishwa.
Amesisitiza kuwa ni wajibu wa vikao husika kuwachuja wagombea kwa misingi ya sifa, uwezo na maadili, badala ya kufuata ushawishi wa muda mfupi au makundi ya maslahi.
Akitumia maneno yenye uzito mkubwa, Dkt. Samia ameweka bayana kuwa CCM haitaki kuwa chama cha watu wanaotafuta tu madaraka bila maono wala maadili ya kiuongozi.
Amesema kuwa kuwapitisha wagombea wasiostahili ni kuhatarisha mustakabali wa chama.
"Vikao vinavyokwenda kuchuja watu , vinavyokwenda kuchuja wagombea wakatende haki, anayefaa aambiwe anafaa , asiyefaa tuseme huyu anakasoro , hatufai huko mbele tunapokwenda, tukitoa mwanya na kupitisha wanaotafuta tu na mimi niwemo ndiyo tunapata wale waokwenda huko, Chama kinakuwa Gwajimanised, kwahiyo tusigwajimanise Chama chetu, Magwajima tuyaache nje”,amesema Dkt. Samia.
Kauli hii inatafsiriwa na wachambuzi wa siasa kama mwendelezo wa msimamo wa Dkt. Samia wa kujenga CCM imara, yenye viongozi waadilifu, wenye uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa maslahi ya wananchi, badala ya kujaza nafasi kwa mantiki ya urafiki au mihemko ya kisiasa.
Social Plugin