
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera, Mhandisi Ntuli Mwaikokesya
Na Lydia Lugakila, Bukoba
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Kagera imeendelea kutoa tahadhari kwa wafanyabiashara wanaofanya biashara pembezoni mwa barabara kwani wapo
hatarini endapo ikitokea ajali za barabarani zisizotarajiwa.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera, Mhandisi Ntuli Mwaikokesya, ametoa kauli hiyo wakati akizungumzia masuala mbalimbali yanayohusiana na usalama barabarani, hasa katika kipindi hiki cha mvua.
Mwaikokesya amesisitiza kuwa, kwa mujibu wa sheria ya barabara, hairuhusiwi mtu kufanya shughuli yoyote ndani ya hifadhi ya barabara.
Ameonya kuwa, endapo ajali itatokea, wafanyabiashara walioko pembezoni mwa barabara hawatakuwa salama.
"Ni muhimu kwa Wananchi kutokaa kwenye hifadhi ya barabara, ndiyo maana kuna maeneo yaliyotengwa," amesisitiza.
Aidha, Mhandisi Mwaikokesya amewasihi madereva kuzingatia alama za barabarani na kufuata maelekezo yanayotolewa.
Pia Ameeleza kukerwa na tabia ya baadhi ya madereva wanaoshindwa kufuata kisheria kuhusu maeneo yasiyoruhusiwa kupita.
Amefafanua kuwa maeneo ambayo yamewekwa kisheria kwa ajili ya ustawi wa barabara ni muhimu kwa ujenzi na matengenezo ya barabara, hivyo ni marufuku kufanya shughuli nyingine kama biashara katika maeneo hayo.
"Ni muhimu kuhifadhi na kuheshimu barabara hizo," amesisitiza Meneja huyo.
Mhandisi Mwaikokesya ametoa ahadi kwa Wananchi wa Kagera kuwa mvua zinazonyesha haziwezi kuwa sababu ya wasiwasi kwani wataalam wa TANROADS wako tayari kuhakikisha barabara zinabaki salama na matumizi yake yanaendelea kwa haraka.
Hata hivyo ameongeza kuwa, kwa muda usiozidi masaa 48, barabara zitakapokatika kutokana na mvua, watahakikisha zinarejeshwa ili kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao.
Social Plugin