VIKUNDI 42 VYA WATU WENYE ULEMAVU VYAJIIMARISHA KIUCHUMI KUPITIA iSAVE KIJALUBA


Wanachama Wanufaika na Mafunzo na Mikopo 

Jumla ya shilingi milioni 143,077,862 zimekusanywa katika mzunguko wa kwanza wa mwaka mmoja kwa vikundi 42 vya kuweka na kukopa vya iSAVE KIJALUBA kutoka katika Wilaya ya Kusini Unguja na Wilaya ya Chakechake Pemba ambapo fedha hizi zinajumuisha hisa zilizowekwa, pesa za mfuko wa jamii na faida kutoka katika ada ya usimamizi ya uchukuaji wa mikopo.


 Vikundi hivyo vina jumla wanachama 1,186 wakiwemo watu wenye ulemavu 811 ambao ni sawa na asilimia 68 ya wanachama wote ambapo kati ya hao 811 wanawake ni 422 na wanaume ni 389. 


Katika kipindi cha mwaka mmoja vikundi hivi vimepatiwa elimu mbalimbali ikiwemo elimu ya kuendesha biashara, elimu ya kuweka akiba na kukopa pia utengenezaji wa bidhaa mbalimbali ikiwemo sabuni, achari, ushonaji wa mikoba ya ukili na hata ukulima wa mbogamboga, ambapo biashara hizi kwa kiasi kikubwa zimewasaidia kujikomboa kiuchumi na wanaziendesha kwa kupitia mikopo ambayo wanaichukua ndani ya vikundi vyao. 


Wanavikundi wa iSAVE KIJALUBA wanajivunia vikundi hivyo kwa kuwa vimewapa muamko wa kujitegemea na kuwasaidia katika shughuli mbalimbali ikiwemo kusomesha watoto wao, kuendeleza biashara, mahitaji ya nyumbani na mengineyo, pia kuweko kwa mfuko wa jamii umewasaidia katika maafa, misiba na mambo mengine ya kijamii. 


“Kikundi hichi kinatusadia sana na tunajivunia khasa, tunafanya biashara, tunakopa na maisha yamebadilika sivo kama yalivyokuwa, tunashukuru sana kwa kuanzishiwa vikundi hivi”, anasema Asha Amour mwanakikundi cha “nyota ya bahati” kilichopo Bwejuu. 


Kutokana na umuhimu na faida ya kuweka akiba, baadhi ya vikundi wamepandisha hisa zao kutoka shilingi 500 hadi shilingi 1000 na wengine kutoka 1000 hadi 2000 kwa hisa moja, hii ni kuonesha maendeleo na ukuwaji wa wanavikundi hao ambapo mwanzoni kutokana na hali zao za kiuchumi hawakutegemea kama wangeweza kumudu hata hiyo shilingi 500 kwa hisa.


 “Mwanzoni jamii na sisi wenyewe tulikua tuna mtazamo kwamba hatuwezi kuweka akiba, na ilikua ni ngumu hata kuingia katika vikundi hivi kutokana na kukosa hiyo shilingi 500 ya hisa, lakini baada ya kuingia na kumalizika mzunguko wa mwanzo ile pesa tuloipata ilitusaidia sana, kwa hivyo tukakubaliana na wenzangu kwamba madhali tushakua na biashara ndogo ndogo na ili faida iwe kubwa mwisho wa mwaka, ni lazima tuongeze hisa kutoka shilingi 1000 hadi shilingi 2000”, anasema Maryam Said ambae ni mshika fedha wa kikundi cha “Tukiwezeshwa Tunaweza” kilichopo Mbuzini Pemba. 


Vikundi hivi vimeanzishwa ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa iSAVE KIJALUBA wenye lengo la kuwakomboa watu wenye ulemavu kiuchumi ambao unatekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ) na Shirikisho la Jumuiya za Watu wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA), kwa ushirikiano mkubwa na Jumuiya ya Watu wenye Ulemavu ya Norway (NAD).

 Dr. Mzuri Issa 

Mkurugenzi TAMWA ZNZ.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post