MSAJILI WA HAZINA AZIUNGANISHA KAMPUNI YA MAJI SONGWE (SOWACO) KWENDA MAMLAKA YA MAJI MBEYA (WSSA)

 
Mwandishi Wetu Mbeya.

Katika kutimiza wajibu wake wa kisheria katika usimamizi wa uwekezaji wa umma hususani kutunza mali za Serikali, Ofisi ya Msajili wa Hazina ilibaini kwamba kuna uwalakini katika usimamizi na uendeshaji wa kampuni ya Maji Songwe (SOWACO) hivyo ilitoa mapendekezo kwa Mamlaka kuiweka kampuni hii chini ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Mbeya WSSA).


Mei 2021 Ofisi hiyo iliomba idhini kwa Katibu Mkuu Kiongozi aridhie uhamishwaji wa SOWACO kwenda Mbeya-WSSA ambapo Julai 3,2023 ombi hilo lilikubaliwa.

Akizungumza jana Mei 31,2024 Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu amesema malengo makubwa ya Serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2025/26, asilimia 85 wakazi wa vijijini na asilimia 95 wa Mjini wanapata huduma ya maji safi na salama kwa kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2030.

"Kuhamishia shughuli za SOWACO Mbeya WSSA sio tu itasaidia kuongeza thamani za mamlaka, kuongeza wigo wa wateja na mapato, bali pia ni kutimiza adhma hii kubwa ya serikali ya kuongeza maji safi na salama pamoja na kuboresha utoaji wa huduma ya maji katika eneo la songwe na Mkoa wa Mbeya kwa ujumla," amesema Mchechu.

Kwa mujibu wa taarifa ya tathimini ya mali za SOWACO, mali zenye jumla ya thamani ya Sh 985 milioni zimehamishwa kutoka SOWACO kwenda Mbeya WSSA, mali hizo zinajumuisha ardhi yenye thamani ya Sh 175 milioni, majengo Sh 366 milioni, mashine na mitambo Sh 439 milioni.

Amesema takwimu za ufuatiliaji za OMH zimeonyesha Mbeya WSSA inafanya vizuri katika utendaji wake katika kipindi cha miaka minne cha kuanzia mwaka 2019/20 hadi 2022/23 mapato yaliongezeka kwa asilimia 14 kutoka Sh 12.7 bilioni mwaka 2019/20 hadi Sh 14.5 bilioni kwa mwaka 2022/23.

"Ongezeko hili sio kubwa na nina imani kuwa mamlaka inaweza ikafanya vizuri zaidi kwa kuzalisha maji, wigo wa wateja hivyo mapato yataongezeka na kuifanya mamlaka kuwa na uwezo endelevu wa kifedha," amesema.

Aidha, amesema mamlaka ina nafasi nzuri zaidi na wigo mpana wa kuongeza ufanisi katika misingi ya kibiashara na kwa kuzingatia vigezo mahususi vya kiutendaji vilivyowekwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Katika kuhakikisha kunakuwa na usimamizi makini kwa taasisi za umma, ofisi yake imepitia upya na kuboresha vigezo vya utendaji kazi vinavyozingatia aina ya sekta na majukumu yanayofanywa na taasisi.

Hivyo, amesema kwa Mamlaka za maji vigezo vya msingi vya kupima utendaji wake ni utendaji wa kifedha unaojumuisha ziada, ukwasi, ufanisi na uendelevu pamoja na mchango katika mfuko mkuu wa Serikali.

"Mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira zinatoa huduma, asili ya majukumu yake ni biashara na zinatakiwa kuwa na faida au ziada ili kuongeza na kuboresha miundombinu yake,"amesema Mchechu na kuongeza kuwa "Mbeya-

WSSA ikijengewa misingi thabiti na endelevu ya kiutendaji zitafanya vizuri na kuweza kutengeneza ziada ya kutosha kuendeleza miradi mikubwa ya maji na hatimaye kupunguza utegemezi serikalini,"

Hata hivyo, amewataka mamlaka za maji kutumia vyanzo mbadala vya fedha za kutekeleza miradi mikubwa ya maji kama ilivyo kwa Tanga- WSSA ambao wameweka historia ya kukusanya Sh 54.7 bilioni sawa na asilimia 103 kwa kuuza hati fungani ya kijani (Tanga green bond), na kuvuka malengo waliyojiwekea ya kukusanya Sh 53.120 bilioni.
  

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post