MHE. SAGINI : MAWAKILI WA SERIKALI TUISHAURI IPASAVYO SERIKALI


Na Hyasinta Kissima-WKS

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini amewataka Mawakili wa Serikali kuishauri ipasavyo Serikali na Taasisi zake wakiwemo Viongozi kuhusu namna ya kushughulikia na kumaliza migogoro na Wananchi au Wawekezaji bila kuathiri maslahi ya Nchi.

Mhe. Sagini ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo kwa Mawakili wa Serikali yanayofanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia Mei 20, 2024, Lush Hotel Jijini Arusha.

"Kwenye eneo hili napenda kuwashauri kuwa more 'proactive rather than reactive' mtakapoona Viongozi wetu katika utendaji wao kuna dalili ya kuleta migogoro kwenye utekelezaji wa mikataba, msisubiri mambo yaharibike. Ninyi Mawakili wa Serikali mpo, mkisubiri yakaharibika watu wakaenda kwenye vyombo vya kutoa haki kama Mahakama au Mabaraza ya Usuluhishi ya ndani na nje ya nchi maana yake kazi imeanza kuwa ngumu.Lakini kama tungewahi tukatoa ushauri mapema tungezuia hali isiwe mbaya",Alisema Naibu Waziri Sagini.

Aidha, ameipongeza Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa mafanikio makubwa ikiwemo kuitetea Serikali katika mashauri ya madai na usuluhishi jambo ambalo limepeleka kuokoa fedha nyingi za Serikali katika kipindi kifupi tangu kuanzishwa kwa ofisi.


Aliendelea kusema, matumaini ya Wizara ya Katiba na Sheria Mawakili hao kuendelea kuyatumia mafunzo hayo kama chachu katika kuendeleza mafanikio hayo na kuwafanya kutoridhika bali kuamsha ari mpya katika kuyaishi na kuyaendeleza kwa faida ya Serikali, Nchi na Wanachi.


Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende aliainisha ajenda kuu tatu katika mafunzo hayo ambapo ajenda ya kwanza ikiwa ni uzinduzi wa nembo ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambayo itatumika kama utambulisho katika mawasiliano mbalimbali, ajenda ya pili ikihusisha mafunzo kwa Mawakili wa Serikali yayohusu uwasilishaji wa mada mbalimbali na majadiliano na ajenda ya tatu ikiwa ni kufanya tathmini ya namna ambavyo Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Serikali zimefanikisha kuendesha na kuratibu uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi nje na ndani ya nchi.


Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali tangu mwaka 2020 imekuwa na utaratibu wa kua ndaa mafunzo kwa Mawakili wa Serikali ili kuongeza maarifa na ujuzi zaidi katika maeneo mtambuka ambayo Mawakili hujishughulisha nayo ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kwa weledi mkubwa ambapo kwa mwaka 2024, jumla ya Mawakili 500 kutoka Wizara zote Nchini,Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Zanzibar, Taasisi za Umma, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Taifa, Wakala wa Serikali, Mashirika ya Umma, Mamlaka za Udhibiti na Vyuo mbalimbali hapa Nchini wameshiriki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post