EWURA : WAFANYABIASHARA YA MAFUTA ZINGATIENI TARATIBU

Meneja wa Mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati na Maji ( EWURA ) Kanda ya Ziwa , George Mhina akizungumza wakati wa semina na maafisa biashara pamoja na wadau

Na Mariam Kagenda _Kagera

 Wafanyabiashara ya Mafuta mkoani Kagera wametakiwa kuhakikisha wanazingatia sheria kwa kufata kanuni na taratibu na Mafuta wanayoyauza yawe yamelipiwa kodi na kuwekewa vinasaba.

Meneja wa Mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati na Maji(EWURA) Kanda ya Ziwa, George Mhina  amesema hayo wakati wa Semina ya kutoa elimu kwa umma kuhusiana na kazi na wajibu wa Mamlaka hiyo ambayo imefanyika katika ukumbi wa ELCT katika Manispaa ya Bukoba.

Mhina amesema kuwa Mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati na Maji (EWURA) imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara hasa katika maeneo ya  wilaya  zilizoko pembezoni kama Ngara na Misenye kuhakikisha mafuta yanayotumika Tanzania ni yale  yaliyolipiwa  kodi na yana vinasaba.


Ameongeza kuwa wanapopima na kukuta yale mafuta hayana vinasaba wamekuwa wakichukua hatua stahiki ikiwemo kuwatoza faini na wakati mwingine kuwafungia vituo vyao vya mafuta .


Kwa upande wao baadhi ya wadau wa Mamlaka hiyo walioudhuria semina wamesema kuwa kuna wakati mafuta yanakuwa changamoto jambo ambalo linawadhoofisha wafanyabiashara ambapo wameiomba Mamlaka hiyo kutoa elimu kwa  wafanyabiashara wa mafuta ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu utunzaji wa Mafuta .


Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Siima kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Kagera wakati akifungua semina hiyo amesema kuwa  kati ya wajibu wa mamlaka  hiyo ni kuhakikisha  mafuta ya Petrol Diesel na mafuta ya Taa yanapatikana kwa ubora na gharama stahiki ili fedha hizo ziendelee kutoa mchango wake katika ustawi wa uchumi wa nchi.


Amewahimiza maafisa biashara kuhakikisha wanashirikiana na Ewura jambo ambalo litasaidia  wananchi kupata huduma kwa gharama stahiki ili kutovuruga shughuli za kiuchumi na kuongeza kuwa mamlaka hiyo ina changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na baadhi ya wawekezaji kujenga vituo vya mafuta bila kuwa na vibali vya ujenzi vinavyotolewa na Ewura na kuuza bei ya juu kuliko ile iliyoidhinishwa .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post