SERIKALI KUTUMIA BILIONI 841.19 UJENZI WA BARABARA ZA WILAYA

Na. Catherine Sungura-Dodoma

Katika mwaka 2024/25, Ofisi ya Rais - TAMISEMI imepanga kutumia shilingi bilioni 841.19 kwa ajili ya ujenzi, matengenezo na ukarabati wa miundombinu ya barabara za wilaya.

Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 257.03 ni za Mfuko wa Barabara, shilingi bilioni 127.50 Mfuko Mkuu wa Serikali, shilingi bilioni 325.77 ni za tozo ya mafuta (shilingi 100 kwa lita), shilingi bilioni 4.03 za mapato ya ndani kupitia Wakala ya Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam na shilingi bilioni 126.85 ni fedha za nje. 

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, OR-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya  Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa  Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Alisema fedha hizo zitaenda kutekeleza matengenezo na ukarabati wa barabara za wilaya zenye urefu wa Km 20,745.31, ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa Km 434.50 pamoja na ujenzi wa barabara za changarawe zenye urefu wa Km 13,802.34.

Aidha, ujenzi wa madaraja 160 na ukarabati wa madaraja 21, ujenzi na matengenezo ya boksi kalavati 586 na vivuko (drifti) 15, ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua yenye urefu wa mita 141,070.54, ujenzi wa kingo za Mto Msimbazi, kudhibiti maeneo ya juu ya Mto Msimbazi (upstreams) pamoja na kuhamisha karakana ya mabasi yaendayo haraka kutoka Jangwani kwenda eneo la Ubungo Maziwa.

Waziri Mchengerwa aliongeza fedha hizo zitaenda kuboresha miundombinu shindanishi katika Miji Tanzania (TACTIC) kwa kujenga miundombinu katika Halmashauri 12 za Majiji ya Dodoma, Arusha, Mwanza na Mbeya, Halmashauri za Manispaa ya Kigoma, Songea, Ilemela, Kahama, Morogoro, Sumbawanga na Tabora na Halmashauri ya Mji Geita. 

Pia miundombinu msingi inajumuisha ujenzi wa masoko, mitaro ya maji ya mvua, stendi za mabasi, maghala ya kuhifadhia mazao na kujenga barabara kiwango cha lami Km 147.5, kuondoa vikwazo vya upitikaji barabarani kwenye wilaya 131 na ujenzi wa barabara kiwango cha lami Awamu ya Pili Km 164 kupitia Programu ya Kuongeza Fursa za Kiuchumi na Kijamii Nchini (RISE) pamoja na ujenzi wa barabara zenye urefu wa Km 250, kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam Awamu ya 2 ambapo kati ya hizo Km 132 zimefanyiwa usanifu.

Kwa upande wa matumizi ya teknolojia mbadala kwenye ujenzi wa miundombinu, Waziri huyo alisema kwa Mwaka 2024/25 Ofisi ya Rais- TAMISEMI kupitia TARURA  imepanga kuendelea na majaribio ya matumizi ya teknolojia mbadala kwenye ujenzi wa miundombinu ya barabara katika Mikoa ya Pwani, Iringa, Dodoma na Simiyu ambapo jumla ya Km 54.15 zitajengwa kwa kutumia teknolojia ya "Ecoroads".


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post